Jaji jimbo la Hawaii azuia marufuku ya Trump kwa muda zaidi

Maandamano dhidi ya marfuku ya Trump Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wanaopinga marufuku hiyo ya Marekani waliandamana miji mingi Marekani

Jaji katika mahakama moja jimbo la Hawaii ametoa agizo la kuzuia kwa muda usiojulikana utekelezaji wa marufuku mpya ya usafiri iliyotangazwa na Rais Donald Trump.

Uamuzi wa Jaji Derrick Watson una maana kwamba Bw Trump atazuiwa kutekeleza marufuku yake ya kuzuia raia kutoka nchi sita zenye Waislamu wengi kuingia Marekani hadi kesi dhidi ya marufuku hiyo imalize kusikizwa.

Katika kesi iliyowasilishwa na jimbo hilo, serikali ya jimbo inasema marufuku hiyo itadhuru utalii na pia kuzuia uwezo wake kuwapokea wanafunzi na wafanyakazi kutoka nchi za nje.

Rais Trump alikuwa amesema marufuku yake mpya ingewazuia magaidi kuingia Marekani.

Jaji Watson alitoa uamuzi wake Jumatano baada ya kuwasikiliza mawakili wanaowakilisha serikali ya jimbo la Hawaiii na Wizara ya Haki Marekani.

Jaji huyo amegeuza uamuzi wake kutoka kuwa kuzuia kwa muda mfupi hadi kuwa kuzuia kwa muda usiojulikana, hadi kesi hiyo isikilizwe na uamuzi kutolewa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Jaji Watson amegeuza uamuzi wake kutoka kuwa kuzuia kwa muda mfupi hadi kuwa kuzuia kwa muda usiojulikana

Agizo lililokuwa limetolewa na Trump, ambalo lilifaa kuanza kutekelezwa usiku wa kuamkia 16 Machi, lingepiga marufuku kwa miezi mitatu raia kutoka nchi sita zenye Waislamu wengi kuzuru Marekani.

Mataifa hayo ni Iran, Libya, Syria, Somalia, Sudan na Yemen.

Aidha, ingezuia wakimbizi kuingia Marekani kwa kipindi cha siku 120.

Bw Trump amesisitiza kwamba hatua hiyo inalenga kuzuia magaidi wasiingie Marekani lakini wanaoipinga wamesema inabagua makundi ya watu.

Marufuku nyingine ya awali aliyokuwa ameitoa Januari ilisababisha mtafaruku na maandamano kabla ya kuzuiwa na jaji mjini Seattle.

Hawaii ni mojawapo ya majimbo kadha ya Marekani yanayopinga marufuku hiyo.

Mawakili wa jimbo hilo waliambia mahakama kwamba marufuku hiyo inakiuka katiba ya Marekani kwamba watu hawafai kubaguliwa kwa misingi ya asili yao.

Jimbo hilo pia limesema marufuku hiyo itaathiri utalii na uwezo wa serikali ya jimbo hilo kupokea wanafunzi na wafanyakazi kutoka mataifa ya nje.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii