Rais wa zamani Korea Kusini Park Geun-hye akamatwa

Park Geun-hye Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bi Park amepelekwa kizuizini Seoul

Rais wa Korea Kusini aliyeondolewa madarakani wiki chache zilizopita Park Geun-hye amekamatwa na kuzuiliwa kuhusiana na tuhuma za rusha ambazo zilichangia kutimuliwa kwake kutoka madarakani.

Park, 65, alisafirishwa kwa gari hadi kwenye kituo cha kuwazuilia watuhumiwa wa uhalifu kusini mwa Seoul baada ya mahakama kuidhinisha kukamatwa kwake.

Bi Park anatuhumiwa kumruhusu rafiki yake wa karibu Choi Soon-sil kudai pesa kwa lazima kutoka kwa kampuni kubwakubwa.

Bi Park amekanusha madai hayo.

Rais huyo wa zamani aliomba radhi kwa umma wiki iliyopita, kabla ya kuhojiwa na maafisa wa mashtaka kwa saa 14.

Waendeshaji mashtaka walisema Jumatatu kwamba "wameamua kwamba ni vyema, kwa kufuata sheria na maadili nchini humo, kuomba kibali cha kumkamata".

Walisema ushahidi, ambao unapatikana katika diski za kompyuta huenda ungeharibiwa iwapo Bi Park hangekamatwa.

Bi Choi amefunguliwa mashtaka ya ulaji rushwa na tayari kesi dhidi yake imeanza.

Bi Park ndiye rais wa tatu wa zamani Korea Kusini kukamatwa kwa tuhuma za kuhusika katika uhalifu, shirika la habari la Yonhap limeripoti.

Mahakama ya Seoul ilitoa kibali cha kukamatwa na kuzuiliwa kwa Bi Park anapoendelea kuchunguzwa kuhusu ulaji rushwa, kutumia vibaya mamlaka, kutumia mamlaka yake kushinikiza watu na kuvujisha siri za serikali.

Uamuzi wa mahakama ulitolewa baada ya kikao cha mahakama kilichodumu saa tisa Alhamisi. Bi Park alihudhuria kikao hicho.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Wafuasi wa Bi Park walikusanyika nje ya nyumba yake alipokuwa mahakamani

Video zilionyesha Bi Park akiwa amebebwa kwa gari jeusi aina ya sedan na kusafirishwa hadi kizuizini.

Licha ya kwamba ilikuwa mapema sana asubuhi, wafuasi wake karibu 50, wakiwa na bendera za taifa hilo na wakiitisha kuachiliwa kwake, walimsubiri langoni, shirika la habari la AFP linaripoti.

Bi Park anaweza kuzuiliwa kwa hadi siku 20 kabla ya kushtakiwa rasmi.

Akipatikana na hatia, anaweza kufungwa kifungo cha hadi miaka 10 jela.

Hwang Kyo-ahn, wambaye ni mwaminifu kwa Bi Park, kwa sasa ndiye kaimu rais.

Uchaguzi utafanyika tarehe 9 Mei.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii