Stellar Daisy: Wasiwasi kuhusu meli ya Korea Kusini iliyotoweka

Stellar Daisy mwaka 2014 Haki miliki ya picha NSRI
Image caption Stellar Daisy ilipokuwa kwenye operesheni ya kuokoa baharia mgonjwa karibu na Afrika Kusini mwaka 2014

Maafisa wa uokoaji wanasema hawajapata mafanikio yoyote katika kuwatafuta manusura wa meli kubwa ya Korea Kusini ambayo ilizama kusini mwa bahari ya Atlantiki.

Ni mabaharia wawili pekee ambao wameokolewa kutoka kwa meli hiyo kwa jina Stellar Daisy, ambayo taarifa zinasema huenda ilizama Ijumaa.

Juhudi za uokoaji zimefanikiwa kupata mafuta, vifusi na mashua za uokoaji zikiwa hazina watu ndani, duru katika serikali ya Korea Kusini ziliambia shirika la habari la Yonhap.

Meli hiyo kubwa ya kusafirisha mizigo ilikuwa imewabeba wahudumu 24.

"Muda unavyoendelea kusonga ndivyo matumaini ya kupata manusura yanavyoendelea kufifia," Gaston Jaunsolo, msemaji wa jeshi la wanamaji la Uruguay aliambia Reuters.

Meli hiyo ilizama eneo la bahari kilomita 3,7000 kutoka pwani ya Uruguay.

Meli hiyo ilimilikuwa na kampuni ya Polaris lakini ilisajiriwa katika visiwa vya Marshall.

Ilikuwa na raia 16 wa Ufilipino na wanane wa Korea Kusini ilipozama.

Ilikuwa ikisafirisha tani 260,000 za mchanga wenye madini ya chuma kutoka Brazil hadi China.

Mara ya mwisho mawasiliano kupokelewa kutoka kwa meli iliyo ilikuwa Ijumaa baharia mmoja alipotuma arafa kwa mmiliki wa kampuni ya Polaris akisema ilikuwa inazama.

Bw Jaunsolo aliambia wanahabari kwamba meli hiyo ilipasuka mara mbili kisha ikazama.

Mabaharia wawili kutoka Ufilipino walipatikana kwenye mashua moja ya uokoaji Jumamosi.

Waliambia maafisa wa Uruguay kwamba wakati mmoja, nahodha aliwaonya mabaharia kwamba majji yalikuwa yakiingia kwenye meli na kwamba meli hiyo ilikuwa inapasuka.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii