Mauaji ya washukiwa wa uhalifu kuchunguzwa Kenya

Mauaji ya washukiwa wa uhalifu kuchunguzwa Kenya Haki miliki ya picha The Star, Twitter
Image caption Mauaji ya washukiwa wa uhalifu kuchunguzwa Kenya

Mkuu wa polisi nchini Kenya Joseph Boinet ameamrisha kufanywa uchunguzi kufuatia video moja ambayo ilisambazwa kwa wingi mitandaoni, ikimuonyesha mwanamume ambaye anatajwa kuwa afisa wa polisi, akimuua kwa kumpiga risasi kijana mmoja katika mtaa wa Eastleigh kwenye mji mkuu wa Nairobi.

Video hiyo ya dakika moja inamuonyesha mwanamume aliyekuwa na bunduki mkononi akimshika kijana mmoja shati, ambaye alitajwa kuwa mshukiwa na kukashuka majibizano makali.

Kisha kijana huyo aliamrishwa kulala chini kando na maiti nyingine iliyokuwa imeloa damu, inayotajwa kuwa ya mshirika wake ambaye tayari alikuwa ameuawa, ambapo alipigwa risasi karibu mara nne.

Msemaji wa polisi Charles Owino, alisema kuwa polisi wanajaribu kumtambua mwanamume ambaye alimuua kijana huyo.

Lakini kamanda wa polisi mjini Nairobi Japhet Koome, alisema siku ya Jumamosi kuwa video hiyo ilikuwa imeigizwa.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yamewalaumu polisi na kutaka uchunguzi huru kwa kisa hicho.

Ripoti iliyotolewa na shirika la Amnesty Internationala mwezi Februari, iliiorodhesha Kenya kuwa moja ya nchi yenye visa vingi zaiidi vya mauaji ya kiholela yanayofanywa na polisi.