Klabu yafungwa kwa kucheza muziki wa 'Adhan' Tunisia

Klabu
Maelezo ya picha,

Klabu

Klabu moja nchini Tunisia imefungwa baada ya kanda ya video kutokea ikionyesha DJ akicheza mziki uliyochanganywa na Adhan, maafisa wakuu nchini Tunisia walisema.

Kanda hiyo ya video iliosambazwa siku ya Jumapili kutoka tamasha la Orbit katika eneo la kaskazini mashariki mwa mji wa Nabeul imezua hisia kali katika mitandao ya kijamii.

Gavana wa Nabeul, Mnaouar Ouertani alisema kuwa Klabu hiyo itabaki kufungwa hadi pale taarifa zaidi zitakapotolewa kuhusiana na hatma yake.

Uchunguzi umeanzishwa kuhusu kisa hicho.

Kanda hiyo ya video inaonyesha watu waliokwenda kujivinjari katika tamasha hilo siku ya Ijumaa wakicheza densi ya muziki uliokuwa ukichezwa na DJ wawili kutoka bara Ulaya, karibu na hoteli maarufu, Hammamet, ilio ufuoni mwa bahari.

Mziki huo ulijumuisha aina ya densi iliyochanganywa na Adhan, mwito wa Waislamu kwa maombi, mara tano kwa siku.

" Baada ya kuthibitisha ukweli wa mambo, tuliamua kuifunga klabu hiyo" Bwana Ouertani alikariri

Alisema kuwa meneja wa klabu hiyo amewekwa kizuizini "kwa kukiuka maadili mema yaliozua hisia kali kutoka kwa umma" huku akiongezea kuwa uchunguzi ungali unaendelea.

"Hatutaruhusu mashambulizi dhidi ya hisia za kidini" alisisitiza Bwana Ouertani

Siku ya Jumatatu, waandaji wa tamasha la Orbit waliomba msamaha katika ukurasa wao wa facebook, lakini walisema kuwa hawatokubali kujipa jukumu la kuchezwa kwa muziki wa kupotosha.

DJ "hakujua kwamba ingewakera waliohudhuria kutoka nchi ya Kiislamu kama yetu," walielezea katika ujumbe wao katika mtandao wa kijamii kwa lugha ya kifaransa.

Dax J, aliyecheza Adhan, baadaye aliomba msamaha kwa yeyote yule aliyekerwa na muziki alioucheza katika tamasha la Orbit nchini Tunisia siku ya Ijumaa.

"Haikuwa kupenda kwangu kufadhaisha mtu yeyote," Aliongeza.