Uteuzi wa Kitila Mkumbo wazua mjadala Tanzania

Tanzania Haki miliki ya picha Google
Image caption Profesa Kitila Mkumbo mwanazuoni nchini Tanzania

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo, ambaye aliwahi kumtaka Rais John Magufuli kuacha kuondoa wasomi na kuwapa madaraka, ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, uteuzi aliouelezea kuwa ni heshima lakini wa "mshtuko, mshtuko".

Wakati Profesa Kitila akikabiliana na msimamo wake, Rais Magufuli amebadili ahadi yake aliyoitoa Zanzibar aliposema kuwa kiongozi wa upinzani hatatia mguu ndani ya Serikali yake.

Mambo hayo mawili yametokea baada ya Rais kufanya mabadiliko madogo katika safu ya makatibu wakuu.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais nchini Tanzania imeeleza kuwa Profesa Kitila anaenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhandisi Mbogo Futakamba ambaye amestaafu.

"Ni shock, shock, shock (mshtuko), sikutegemea na nashindwa hata kukuelezea . Ni heshima kubwa sana aliyonipa Rais," alisema Profesa Kitila, ambaye ni muasisi na mshauri wa ACT Wazalendo, nafasi ambayo alijiuzulu.

Profesa Kitila hakuwa na taarifa ya uteuzi wake hadi alipopigiwa simu na gazeti la Mwananchi.

"Nimerudi jana kutokea Dodoma kwenye uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki pamoja na masuala ya Wizara ya Elimu. Hivi tunavyozungumza niko hapa na mabegi yangu nimetoka nyumbani asubuhi hii nilikuwa najiandaa kuingia katika kipindi hapa chuoni kufundisha," alisema."Haya mambo ni mazito sana nakosa hata namna ya kuelezea."

Profesa Kitila amesema ni heshima kubwa na asiyoweza kuielezea kwa sasa kutokana na imani kubwa aliyoionyesha Rais Magufuli kumuingiza katika safu ya makatibu wake wakuu.

Profesa Kitila aliwahi kunukuliwa akisema kuwa Rais amekuwa akiondoa wahadhiri vyuoni na kuwapa madaraka ya kisiasa na kuviacha vyuo vikipukutisha wasomi.

Alisema vyuo vilivyoathirika sana na uteuzi wa Rais Magufuli ni Chuo kikuu cha Dar-Es-Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma na kumtaka Rais awaache wasomi waendelee kufanya kazi zao, hasa za utafiti ili wasaidie wanafunzi.

Akizungumzia uteuzi huo, kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamepokea kwa mikono miwili taarifa ya uteuzi huo, akisema umeonyesha Rais amebaini kuwa vyama vya upinzani vina uwezo, weledi na uzalendo wa kutumikia nchi.

Alisema ameridhia uteuzi huo baada ya kushauriana na viongozi wakuu wenzake wa chama hicho.

Alisema wamejiuliza mambo mengi, lakini wameamua kumruhusu kwenda kutumikia nafasi hiyo kwa sababu Profesa Kitila alikuwa mtumishi wa umma na kuteuliwa kwake kushika nafasi hiyo ni sawa na kupandishwa cheo kwenye utumishi wa umma

"Wengine waliona kama jambo hili lingetunyong'onyesha kama chama ama ni kufutwa kwa machozi baada ya kukataliwa na kanuni za Bunge kushiriki (uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki), lakini tukaona hatuwezi kuwanyima Watanzania mtu mwenye weledi kuwatumikia," alisema Zitto.

Kwa upande mwingine, Rais amebadili kauli yake kuwa hatateua wapinzani kuingia kwenye Serikali yake.

Ikumbukwe kwamba, mwaka huu akiwa kisiwani Unguja, Magufuli alimshangaa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwa kuteua wanasiasa wa vyama vya upinzani kwenye Serikali yake wakati alipata ushindi mkubwa.

"Sijawahi kuona, makamu mwenyekiti wa Tadea amezungumza hapa, rais uchaguliwe, upate asilimia 92, bado unachukua watu wa vyama vingine unawaingiza kwenye Serikali yako," alisema Rais Magufuli kwenye mkutano wa hadhara.

"Mimi nilipata asilimia 58, hakuna wa chama kingine mle ndani yangu. Na wala hataingia."Mimi nimepata asilimia 58 hakuna atakayekanyaga mguu kwenye Serikali yangu."

Profesa Kitila ni mtu wa pili kutoka vyama vya upinzani kuteuliwa na Rais baada ya mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya msamaha kwa wafungwa.

Kada mwingine wa ACT Wazalendo, Hidaya Usanga aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa mkurugenzi wa Wilaya ya Tarime. Lakini wakati akisubiri kula kiapo Ikulu, Usanga, ambaye katika uchaguzi uliopita aligombea ubunge wa Jimbo la Malinyi kwa tiketi ya ACT Wazalendo, aliitwa pembeni na kutakiwa aondoke.

Uteuzi wa Profesa Kitila umeibua mjadala katika mitandao ya kijamii, huku wasomi wakimjadili.