Yanga yataka uungwaji mkono

Tanzania Haki miliki ya picha Google
Image caption Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa Master

Timu ya Yanga imewaomba Watanzania na wapenzi wa soka kote nchini Tanzania , kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu hiyo katika mechi yao ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria ili kuongeza hamasa ya ushindi.

Wawakilishi hao wa Tanzania wanatarajia kuwakaribisha Waalgeria mwishoni mwa wiki hii kwenye uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika mechi ya kuwania kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa Master, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam kuwa maandalizi ya mechi hiyo yanakwenda vizuri na timu yake imejipanga kushinda , hivyo wanahitaji uungwaji mkono maana wanawaikilisha nchi."Maandalizi ya mchezo yanakwenda vizuri, timu inaendelea na mazoezi ya kujiimarisha kuhakikisha wanashinda. Tunaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuwatia moyo wachezaji na kuwapa nguvu," alisema.Alitaja viingilio vya mchezo huo kuwa ni Sh 5,000 viti vya kawaida, VIP B na C Sh 20,000 na VIP A Sh 30,000.

Aidha Mkwasa alisema bado wana imani na Kocha wao George Lwandamina na hakuna mpango wowote wa kumchukua Kocha wa zamani wa Azam, Stewart Hall kama ambavyo taarifa zimekuwa zikisambaa.

"Timu yetu kwa sasa inaongoza ligi na tupo katika njia nzuri ya kutetea ubingwa wetu. Hawa wanaoleta maneno hawana nia njema na klabu bali wanataka watu waache kufanya kazi ili malengo yao yatimie, klabu haipo katika mpango ambao utaleta hasara na kuanza kulipa fidia,"alisema.

Alisema wapinzani wa Yanga, MC Alger wanatarajiwa kuwasili nchini Alhamisi hii wakitokea kwao Algeria tayari kwa mchezo huo. Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Rwanda.