Profesa ahofia kufutwa baada ya kuchapisha video akinengua kiuno Misri

Mona Prince alichapisha video akinengua kiuno Misri Haki miliki ya picha FACEBOOK/MONA PRINCE
Image caption Mona Prince alichapisha video akinengua kiuno Misri

Profesa mmoja kutoka Misri anahofia kupoteza kazi baada ya kuweka video yake akicheza densi ya kunengua kiuno kwa ukurasa wake wa Facebook.

Video hiyo, pamoja na picha ya Mona Prince akiwa amevalia mavazi ya kuogelea, imesambazwa sana na kuvutia hisia kali kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa sasa profesa huyo ambaye hufunza lugha ya kiingereza na fasihi katika chuo kikuu cha Suez anafanyiwa uchunguzi.

Japokuwa kuna wale waliomtetea, wengi katika mitandao ya kijamii wamesema kuwa walitarajia kuwa profesa wa chuo kikuu kufuata mila za wamisri ambayo ni jamii ya kihafidhina na awe na tabia za kuigwa.

Mkuu wa kitengo anakofunza Bi. Prince, Mona Saba, aliiambia BBC kwamba hakuheshimu mila na desturi za chuo kikuu.

Aliongeza kuwa Bi Prince alikuwa anachunguzwa kwa mambo mengine yakiwemo maswala ya nidhamu, masaa za kwenda shuleni na mafunzo yake pamoja na matokeo ya wanafunzi wake.

Katika kurasa wake wa Facebook, Bi Prince alitupilia mbali maoni ya baadhi ya waliomkashifu akisema kuwa baadhi ya masuala yaliyotajwa yalikuwa ya usimamizi wa chuo na ikiwa inahusishwa na matokeo ya wanafunzi wake, basi makaratasi ya mitihani ipo kukaguliwa na waamue wenyewe.

Alisema kuwa alihofia anaweza kutimuliwa kutoka chuo kikuu lakini ataangalia hatua ya kuchukua huku akishukuru wale waliomuunga mkono. " sitaacha kucheka, kucheza, kuimba na kuandika," alisema kwenye kurasa wake wa Facebook.