Twitter unaishtaki Serikali ya Marekani kuhusu akaunti inayompinga Trump

twitter Haki miliki ya picha Getty Images

Mtandao wa kijamii wa Twitter unaishtaki serikali ya Marekani baada ya kudai ufichue utambulisho wa ukurasa unaompinga Trump.

Ukurasa huo unaofahamika kama @ALT_USCIS ambao haukuwa na maelezo ya utambulisho ulikosoa sera ya uhamiaji ya Bwana Trump.

Mnamo Januari wakati Donald Trump alipokuwa rais, kurasa kadhaa ya mitandao ya kijamii iliyoitwa ''mitandao mbadala" kwa ajili ya huduma za serikali ilianza kuonekana kwenye mtandao.

Mingi ilidai kuanzishwa na waajiriwa wa sasa ama wa zamani katika mashirika hayo, na ilitoa ukosoaji mkali dhidi ya muajiri wao mpya.

Sasa imefichuliwa kuwa utawala wa Trump ulidai Twitter ifichue utambulisho wa walau mmoja miongoni mwa wanaotuma ujumbe huo.

Twitter ilimuomba jaji mjini San Francisco kukataa ombi hilo chini ya sheria za uhuru wa kujieleza.

Hatua hiyo ya Twitter iliungwa mkono na Muungano wa uhuru wa Raia nchini Marekani.