DJ aliyecheza ''Adhan'' katika klabu kufungwa jela

Kazi ya DJ katika klabu ni kuwatumbuiza wateja kwa kucheza mziki waupendao
Maelezo ya picha,

Kazi ya DJ katika klabu ni kuwatumbuiza wateja kwa kucheza mziki waupendao

Mahakama moja ya Tunisia imetoa amri ya DJ wa Uingereza kutumikia kifungo cha mwaka mmoja kwa kucheza muziki uliyochanganywa na Adhan klabuni.

Dax J ni mzaliwa wa London na ameshtakiwa kwa kosa la kukosea maadili ya umma, lakini uamuzi huo ulitolewa wakati ambapo alikuwa tayari ameshatoroka Tunisia baada ya kuomba msamaha.

Klabu aliyocheza muziki huo ilifungwa baada ya kanda ya video kuonesha akicheza mziki uliochanganywa na Adhan . Watu walionyesha kukerwa katika mitandao ya kijamii.

Msemaji wa mahakama alikiambia kituo cha habari cha AFP kuwa mashtaka dhidi ya mmiliki wa klabu na wale walioandaa hafla hiyo yametupiliwa mbali.

Hafla hiyo ilikuwa mojawapo ya tamasha ya Orbit, huko Nabeul na ilikuwa na DJ wawili wa Kiingereza.

Muziki huo ulijumuisha aina ya densi iliyochanganywa na Adhan, wito wa Waislamu kwa ibada, mara tano kwa siku.

"Hatutaruhusu mashambulizi dhidi ya hisia za kidini" alisisema gavana wa Nabeul Mnaoaur Ouertani.

Waandalizi wa tamasha hilo la Orbit waliomba msamaha katika ukurasa wao wa facebook, lakini walisema kuwa hawatokubali kosa la kuchezwa kwa muziki wa kupotosha.

DJ "hakujua kwamba mtindo wake utawaudhi waliohudhuria, wengi ambao wanatokaa nchi ya Kiislamu kama hii yetu," walielezea katika ujumbe wao katika mtandao wa kijamii kwa lugha ya Kifaransa.

Dax J, aliyecheza Adhan, aliomba msamaha kwa yeyote yule aliyekerwa na muziki alioucheza katika tamasha hilo la Orbit.

"Haikuwa kupenda kwangu kumkasirisha mtu yeyote," alisema.

Dax J amecheza muziki katika tamasha na vilabu mbalimbali kote duniani ikiwemo tamasha la techno la Awakenings huko Uholanzi na Glastonbury, Uingereza.

Anaendesha studio mjini Berlin ambako pia anafanya kazi kama mhandisi wa sauti.