Urusi yashutumu shambulio la Marekani dhidi ya Syria

Urusi imekasirishwa na hatua ya Washington kushambulia Syria
Image caption Rais Donald Trump wa Marekani kushoto na Vladmir Putin wa Urusi kulia

Urusi imechukizwa na uamuzi wa Marekani wa kuishambulia kambi ya jeshi la anga mjini Homs nchini Syria kwa makombora.

Maafisa wa Marekani walisema kuwa waliilipua kambi hiyo kwani ndiyo iliyotumika kuendeleza shambulizi liliotumia silaha za kemikali yenye sumu katika mji unaodhibitiwa na waasi, ambapo watu kadhaa walipoteza maisha siku ya Jumanne.

Lakini Urusi inaunga mkono serikali ya Rais Bashar al-Assad na imekashifu shambulizi hilo ambalo linadaiwa kuua watu sita.

Shambulio hilo linajiri siku chache tu baada ya shambulio la gesi ya sumu lililolengwa katika mji wa Khan Sheikhoun, mkoa wa Idlib liloua zaidi ya watu 80, wengi wao wakiwa watoto.

Upinzani wa Syria unasema kuwa ni serikali ya Syria iliyotekeleza shambulio hilo lakini serikali ya Assad inapinga haya.

Inadaiwa kuwa sasa Urusi inaweza kufanya uamuzi wa kuboresha mtindo wa Syria wa kulipua makombora.

Kwa muda mrefu Syria ilikuwa na mfumo ulio fana sana wa ulinzi wa anga zake lakini vita ambavyo vimekuwa vikiendelea umeudhoofisha.

Urusi nayo ina mfumo wa kisasa zaidi wa kurusha makombora kutoka ardhini hadi hewani katika kambi yake ya Syria lakini kwa sababu zisizoeleweka hawajaweza kuzuia mashambulizi ya Waisraeli.

Image caption Rais Bashar Al Asaad wa Syria
  • US Imefanya nini?

Kufuatia amri ya rais Donald Trump, meli mbili za kivita za Marekani zimerusha makombora 59 ya kasi kutoka mashariki mwa bahari ya Mediterenia katika kambi ya jeshi la anga la Syria mjini Homs.

Kulingana na Pentagon, walilenga ndege, majumba ya ndege na vituo vya mafuta, na maeneo ya kuweka silaha.

Maafisa wa Marekani wanadai kwamba waliviarifu vikosi vya Urusi kabla ya kutekeleza mashambulizi hayo ya makombora.

Rais Trump alitangaza kuidhinisha shambulio hilo akiwa jimboni Florida alipokuwa anakutana na rais wa China Xi Jinping, na alisema kuwa Rais Assad ni dikteta huku akitaka jamii ya kimataifa kusaidia kumaliza vita nchini Syria.

Vituo vya habari nchini Syria vimesema kuwa watu tisa waliuawa kutokana na shambulizi hilo, wanne wakiwa watoto, lakini BBC haijaweza kudhibitisha hayo.

Marekani imefanya mashambulizi nchini Syria kuanzia mwaka wa 2014 lakini hii ni mara ya kwanza kulenga kikosi cha serikali ya Assad.

Serikali ya Urusi ni mojawapo ya rafiki wa serikali ya Assad na vikosi vyake vimekuwa vikilenga makundi ya waasi kule Syria.

Rais wa Urusi Vladmir Putin anaamini mashambulizi hayo katika kambi ya anga ya Syria yamekiuka sheria za kimataifa na yamevuruga pakubwa mahusiano kati ya Marekani na Urusi.

Moscow imetaja mashambulio hayo kama uchokozi mkali dhidi ya taifa huru.

Msemaji wa rais Putin (Dmitry Peskov) amesema kwamba kando na kukiuka sheria za kimataifa , Washington imesababisha uharibifu mkubwa katika uhusiano na Moscow.

Wizara ya mambo ya nje imetangaza kusitishwa kwa makubaliano na jeshi la Marekani yalioundwa kuzuia mashambulio ya anga ya Syria.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii