Watu 15 wauawa katika mlipuko wa bomu Mogadishu

Shambulizi hilo liliwalenga viongozi wa kijeshi
Image caption Shambulizi hilo liliwalenga viongozi wa kijeshi

Bomu lililokuwa limetegeshwa katika gari limeuwa takriban watu kumi na tano nje ya kambi ya jeshi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Kundi la wapiganaji wa kiislamu la Al Shabaab limekiri kufanya shambulio hilo siku ya Jumapili asubuhi, huku wakimlenga kiongozi wa jeshi la Somalia.

Hili ni tukio la hivi karibuni katika kampeni za wapiganaji hao ambalo inaendelea kuhatarisha usalama wa nchi.

Shambulio hilo limeharibu magari na kujeruhi watu karibu na wizara ya ulinzi mjini Mogadishu.

Image caption Rais Farmajo alitangaza vita dhidi ya Al Shabaab baada ya kuingia madarakani

Mlipuko huo ingawa ulilenga msafara wa maafisa wa ngazi za juu wa jeshi, lakini idadi kubwa ya waliojeruhiwa ni wananchi wa kawaida waliokuwa karibu kwenye gari.

Taarifa zinasema, baadhi ya wanajeshi na walinzi ni miongoni mwa walioathirika.

Kundi la wapiganaji la Al Shabaab limekiri kuhusika na shambulio hilo.

Shambulio hilo linatokea wiki moja tu baada ya Rais wa Somalia Mohamed Farmajo kutangaza vita dhidi ya Al Shabaab lakini pia kutoa siku 60 kwa wapiganaji watakaotubu.

Kundi hilo limesema kauli hiyo ya Rais ilikuwa na lengo la kuridhisha nchi za magharibi.

Vitisho vya Al Shabaab vimeendelea kwa mwezi wa pili tangu Rais Farmajo kuingia madarakani, huku wapiganaji hao wakilengo maafisa wa serikali na vikosi vya Umoja wa Afrika.