Mwanaharakati aliyemtusi Rais Museveni atupwa rumande

Mwanaharakati aliyemtusi Rais Museveni atupwa rumande Haki miliki ya picha FACEBOOK
Image caption Mwanaharakati aliyemtusi Rais Museveni atupwa rumande

Mtafiti katika chuo kikuu cha Makerere Dr Stella Nyanzi amepelekwa rumande hadi 25 Aprili mwaka huu, baada ya kusomewa makosa mawili yakihusika na matumizi mabaya ya kompyuta pamoja na mitandao ya kijamii.

Dr. Nyanzi ni mkosoaji mkuu wa rais Museveni na familia yake na alikamatwa Ijumaa ya wiki iliyopita.

Dr. Stella Nyanzi, anakabiliwa na mashtaka mawili yakiwemo unyanyasaji wa kimitandao ya kijamii kinyume na kifungu 24 cha sheria ya matumizi mabaya ya kompyuta ya mwaka 2011, huku kosa la pili likiwa ni mawasiliano ya kuchukiza kinyume na kifungu 25 cha sheria ya matumizi mabaya ya kompyuta ya mwaka 2011.

Upande wa mashtaka unadai kuwa Dr. Nyanzi, Januari 28, mwaka wa 2017 katika wilaya ya Kampala alitumia kompyuta kuandika katika ukurasa wake wa Facebook unaoitwa Stella Nyanzi, ambako alitoa madai au pendekezo akisema kuwa rais Museveni miongoni mwa mengine ni sehemu ya makalio au matako, jambo ambalo si la kistaarabu au lisilofaa.

Mshtakiwa hakukiri kosa hilo na kuhusu kosa la pili, akitumia mawasiliano ya kelektroniki ambapo kati ya Januari na Machi mwaka 2017 akitumia Facebook, alisambaza ujumbe unaovuruga amani na haki ya rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni.