Urusi yatakiwa kuacha kumuunga mkono Bashar al-Assad

Mamia ya watoto wameathirika na shambulizi la gesi ya sumu
Maelezo ya picha,

Mamia ya watoto wameathirika na shambulizi la gesi ya sumu

Viongozi wa Marekani na Uingereza wamesema kuna fursa ya kuishawishi Urusi kuacha kumuunga mkono kiongozi wa Syria, Bashar al-Assad.

Katika mazungumzo kupitia njia ya jana, Donald Trump na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May, wamesema ushirika na serikali ya Syria hauna manufaa tena ya kimkakati kwa Urusi.

Ikulu ya Marekani imesema chancellor wa Ujerumani, Angela Merkel, amekubali kwamba Rais Assad sharti ashtakiwe.

Mawaziri wa mambo ya nje kutoka mataifa yanayoongoza kwa viwanda duniani maarufu kama G7 wanafanya mkutano wa siku mbili nchini Italia kujaribu kuja na mkakati wa pamoja kuhusu Syria kabla ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani jijini Moscow hii leo.

Maelezo ya picha,

Rais wa Syria Bashar al-Assad amesema hakuna shambulizi la sumu ya gesi lililofanywa na serikali yake

Wakati huo huo, Marekani imesema imeharibu asilimia ishirini ya ndege za kivita za Syria katika shambulizi la wiki iliyopita, ambalo imeanzisha baada ya kubaini kufanyika kwa shambulizi la silaha za kemikali.

Waziri wa ulinzi wa Marekani, James Mattis amesema serikali ya Syria haina uwezo wa kuziweka mafuta ndege zake au kuziongezea silaha katika uwanja wa Shayrat.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Sean Spicer ametahadharisha kwamba, Marekani haitasita kufanya shambulizi iwapo itabainika kutumika kwa silaha la kemikali.

Syria imekataa kutumia silaha hizo huku Urusi ikiielezea hatua hiyo ya Marekani kuwa haina athari yoyote na ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa.