Abiria atolewa kwa nguvu katika ndege ili kutoa nafasi kwa wafanyikazi

Daktari atolewa kwenye ndege kwa nguvu

Chanzo cha picha, TYLER BRIDGES/TWITTER

Maelezo ya picha,

Abiria atolewa kwa nguvu katika ndege ili kutoa nafasi kwa wafanyikazi

Kanda za video zinazoonyesha jamaa mmoja akiondolewa kwa nguvu kutoka kwenye ndege ya shirika la ndege la United zimesababisha malalamiko katika mitandao ya kijamii.

Video hiyo iliyochukuliwa ndani ya ndege hiyo inaonyesha mwanamume akinyanyuliwa kwa nguvu kutoka kiti alichokuwa amekalia na kuvurutwa katika nafasi iliyo katikati ya viti vya ndege.

Ndege hiyo ilikuwa inaelekea Louisville kutoka Chicago.

Kufuatia tukio hilo la jumapili, Shirika la ndege la United limeomba msamaha kupitia mtandao wa twitter likisema kuwa uchunguzi unafanywa kubaini nini hasa kilitendeka.

Video moja ya dakika 50 iliyonakili tukio hilo imesambazwa zaidi ya mara elfu 16 kuanzia Jumapili.

Jayse D Anspach aliyeweka rekodi hiyo kwenye twitter alisema kuwa ndege hiyo ya United ilikuwa imepakia abiria kupita kiasi na iliwataka watu wanne kujitolea na kuwapa nafasi wafanyikazi wa ndege hiyo waliokuwa wamekosa nafasi na wanaodaiwa kuwa na shughuli za dharura za siku iliyofuata.

"Hakuna aliyejitolea kwa hivyo United ikaamua kuchagua na hivyo wakaamua ni daktari huyo kutoka Asia na mkewe ndio watakaoondoka."

"Daktari huyo alitarajiwa kuwa hospitallini siku ifuatayo na hivyo basi akakataa kujitolea," Anspach alisema.

"Dakika kumi baadaye daktari huyo alikimbia ndani ya ndege akiwa amejaa damu usoni huku akilia na kusema, "Ninataka kwenda nyumbani."

Afisa mmoja wa usalama aliyehusika na tukio hilo amepewa likizo ya lazima kulingana na idara ya anga ya Chicago.

Idara hiyo imesema itafuatilia tukio hilo ambalo haliambatani na utaratibu wao wa kuendesha mambo.

Abiria mwingine Audra B. Ridges aliweka video kwenya mtandao wa facebook na imesambazwa na watu zaidi ya elfu 400.

Aliandika: "Tafadhali sambaza video hii. Tuko kwenye ndege hii ya United ambayo ilitoa tikiti za usafiri kwa abiria wengi kuliko inavyofaa. "

"Wamewachagua watu wanaotaka kuwashukisha ili wafanyikazi wao wapate nafasi. "

"Mtu huyu ni daktari anayepaswa kuwa hospitalini asubuhi."

"Hakutaka kutoka. Sote tumechukizwa na kitendo hiki."

Maelfu ya watu wametoa maoni yao kuhusu video hii kwemye mtandao wa facebook.

Mmoja aliandika: "Jambo hili linakera sana."

Mwingine akasema: "Ni huzuni sana kumuona mtu akitendewa unyama huu. Sitaitumia ndege ya United tena kamwe."

"Lakini mwingine alisema: "Lazima kuna jambo jingine tusilolifahamu kuhusu tukio hili. "

Katika taarifa, shirila la ndege la United lilieleza BBC kuwa: "Ndege nambari 3211 kutoka Chicago kuelekea Louisville ilikuwa ina abiria wengi kupita kiasi."

"Baada ya wafanyikazi wetu kuwatafuta watu wa kutoka kwenye ndege kwa kujitolea, mmoja kati yao alikataa kutoka na hapo ndipo maafisa wa usalama walipoitwa."

Mkurugenzi Mkuu wa United, Oscar Munoz , alielezea katika twitter: "Hili ni tukio linalotukwaza sisi sote hapa United."

"Ninaomba msamaha kwa wale ambao wamelazimika kutafutiwa ndege nyingine."

"Timu yetu inafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa ukweli wa yale yaliyotendeka unabainika haraka," alisema.

"Vile vile tunamtafuta abiria huyu ili kuzungumza naye na kutatua shida hii mara moja,"aliongezea.