Gaidi wa Stockholm akiri kutekeleza shambulizi

Polisi wametoa picha hii walipokuwa wakimsaka mshukiwa

Chanzo cha picha, SWEDISH POLICE

Maelezo ya picha,

Polisi wametoa picha hii walipokuwa wakimsaka mshukiwa

Mshambuliaji aliyetumia lori kuwagonga watu mjini Stockholm huko Sweden, amekiri kutekeleza "kosa la ugaidi", hayo ni kwa mjibu wa wakili wake.

Hayo yamefanyika wakati wa kusikizwa kwa kesi ya mtu huyo aliyeko kifungoni.

Rakhmat Akilov, 39 kutoka Uzbekistan, amekiri mahakamani kuwa alihusika na shambulio hilo.

Watu wanne waliuwawa, baada ya lori kugongeshwa duka moja mnamo siku ya Ijumaa.

"Msimamo wake ni kwamba, amekiri kutekeleza uhalifu wa ugaidi, na akakubali kwamba atafungwa gerezani," amesema wakili Johan Eriksson.

Idara ya Polisi nchini Sweden, imesema kwamba Bw Akilov alifahamika vyema na vyombo vya usalama.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Polisi wa Sweden wakipiga doria nje ya mahakama

Rakhmat Akilov: ambaye alikuwa mshukiwa wa shambulio hilo?

Alinyimwa hifadhi ya ukimbizi nchini Sweden na akaanza kuwaunga mkono wapiganaji wa Islamic State (IS), wanasema.

Anasemekana alitoweka kutoka eneo la shambulio hilo, akiwa bado anayo damu na vigae vya glasi, na akakamatwa saa chache baadaye katika kitongoji kimoja kaskazini mwa mji mkuu Stockholm.

Kwa mjibu wa taarifa, alimuacha mke na watoto wanne nchini Uzbekistan, ili kutafuta pesa na kuwatumia nyumbani.

Baada ya kuomba hifadhi ya ukimbizi mwaka 2014, alifahamishwa mwezi Desemba 2016 kuwa, "ana muda wa mwezi mmoja tu kuondoka nchi hiyo", Afisa mmoja wa polisi, Jonas Hysing amesema.

Alitoweka na mwezi Februari mwaka huu, aliwekwa rasmi katika orodha ya watu wanaotafutwa.