Meli ya India yaachiwa na maharamia Somalia

Haramia wa Kisomalia katika eneo la Bahari Hindi
Maelezo ya picha,

Haramia wa Kisomalia katika eneo la Bahari Hindi

Wanajeshi wa Somalia wamenusuru meli moja ya mizigo ya India, ambayo ilitekwa nyara na maharamia mapema mwezi huu, lakini maharamia hao wamekataa kuwaachia huru wafanyikazi 9 kati ya 11, walipokimbilia usalama wao ufukweni.

Wanaaminika wanazuiliwa katika eneo moja karibu na mji wa Hobyo.

Chombo kiitwacho Al Kausar, ni mojawepo ya meli tatu ambazo zimetekwa nyara katika eneo hilo la upembe wa Afrika ndani ya bahari Hindi, tangu visa vya mwisho vya utekaji nyara kuripotiwa katikia maeneo hayo miaka mitano iliyopita.

Mnamo siku ya Jumapili, mabaharia kutoka Indian, Pakistani na China, waliwanasua wafanyikazi wa Tuvalu- meli iliyosajiliwa ambayo ilikuwa imeabiriwa na maharamia.

Wafanyikazi hao wawili waliokolewa walikuwa ndani ya gari ambalo maharamia waliliacha, baada ya kufukuzwa, hayo ni kwa mjibu wa Mohamed Hashi Arabey, naibu rais wa jimbo la Galmudug, ameliambia shirika la habari la Reuters.

Maelezo ya picha,

Ramani ya Somalia

Baada ya Reuters kuwasiliana na maharamia hao, walisema kuwa wataendelea kumshikilia mwanabaharia huyo, hadi pale mamia ya mabaharia wanaozuiliwa nchini India wataachiwa huru.

Uharamia kwenye maeneo ya maji pwani ya Somalia na Yemen, uliongezeka mara dufu mwaka 2011, huku kukitokea zaidi ya mashambulia 200.

Lakini matendo hayo yamepungua pakubwa katika miaka ya hivi karibuni, baada ya kuongezeka kwa doria inayoongozwa na wanajeshi wa majini kutoka mataifa mbalimbali ya dunia, pamoja na uungwaji mkono wa wavuvi wa maeneo hayo wanaoendesha shughuli za uvuvi baharini.

Hata hivyo, sababu iliyowafanya wavuvi wengi wa kisomali kutoroka kutoka maeneo ya pwani, na kuamia kuwa maharamia, yapata mwongo mmoja uliopita, bado ingalipo, amesema mwaandishi habari wa BBC wa maswala ya usalama Frank Gardner.

Kwa sasa Somalia inashuhudia hali mbaya ya ukame, umaskini umeongezeka mara dufu, huku vijana wengi wakiwa bila ajira.