Wasomalia 11 washinda viti katika uchaguzi Finland

Ramani ya taifa la Finland ambapo raia 11 wa Somalia walishinda viti vya uwakilishi katika uchaguzi wa mabaraza
Maelezo ya picha,

Ramani ya taifa la Finland ambapo raia 11 wa Somalia walishinda viti vya uwakilishi katika uchaguzi wa mabaraza

Wasomalia kumi na moja wamechaguliwa katika uchaguzi wa mabaraza nchini Finland uliofanyika siku ya Jumatatu.

Hatua hiyo ni muhimu sana katika uwakilishi wa jamii ya Somalia inayojulikana kuwa miongoni mwa jamii za wachache.

Japo Wasomali ni mojawapo ya jamii ndogo sana nchini Finland ambako walianza kuwasili kwa idadi ya kutajika katika miaka ya 90, ushawshi wao katika ulingo wa kisiasa unaimarika kila uchao.

Wengi wamekuwa wakishiriki zaidi katika maswala ya kisiasa nchini humo na mwaka huu ndio wameweka rekodi mpya ya kufanikiwa kushinda viti vingi zaidi katika serikali za mitaa - baada ya kuibuka na viti 11 vya udiwani vinne kati yake vikiwa katika jiji kuu la nchi hiyo Helsinki.

Idadi ya watu nchini Finland ni milini 5 na karibu watu 18,000 kati ya hao ni Wasomali.

Madiwani wa Finland ni 9,000 nchi nzima , hivyo viti hivyo 11 vya uwakilishi ndio sasa vinashikiliwa na jamii ya Wasomali.

Kama vile katika mataifa mengine uwakilishi katika ngazi ya udiwani hutumiwa kama ngazi ya kuwania kiti cha ubunge. , hivyo baadhi ya hao madiwani wa kisomali nao pia wameonesha nia ya kuwania viti vya ubunge katika uchaguzi wa siku za baadae.

Na si Finland pekee ambako jamii ya wasomali wameonesha utashi wao wa kisiasa wakiwa ugenini au ukimbizini, wapo pia walioshinda viti vya ubunge kaika mataifa mengine ya ulaya kama vile Canada na kwenye uchaguzi wa hivi majuzi Marekani.