Waafrika wanauzwa Libya katika biashara ya utumwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ripoti ya IOM yasema kuwa wahamiaji wa kiafrika wananunuliwa na kuuzwa katika Libya

Raia wa Afrika wanaojaribu kuvuka na kuelekea barani Ulaya, wanauzwa na watekaji wao na kuuzwa katika "soko la utumwa" nchini Libya. Hayo yamesemwa na shirika la kuwahudumia wahamiaji duniani International Organization for Migration (IOM).

Wahasiriwa wameiambia IOM kuwa, baada ya kuzuiliwa na walanguzi wa biashara ya watu au makundi ya wapiganaji, wanapelekwa hadi kwenye viwanja vya mji au kwenye maeneo ya kuegeshea magari na kuuzwa.

Wahamiaji walio na ujuzi kama vile upakaji rangi au ukulima, wanauzwa kwa bei ya juu, kiongozi mkuu wa shirika hilo la IOM nchini Libya ameiambia BBC

Libya imekuwa katika ghasia tangu mwaka 2011 pale wanajeshi wa shirika la kujihami la mataifa ya magharibi-NATO yalipomuondoa madarakani Rais wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption IOM yasema matendo ya "kutisha" dhidi ya wahamiaji inajumuisha kula chakula kidogo, kuuwawa au kuachwa wafe njaa

Kwa mjibu wa IOM, maelfu ya wanaume chipukizi kutoka mataifa ya kusini mwa jangwa la Sahara wameuzwa katika masoko hayo ya utumwa wa binadamu.

Mhamiaji mmoja kutoka Senegal, ambaye jina lake limebanwa ili kumlinda, amesema kuwa amewahi kuuzwa katika masoko kama hayo katika mji wa Sabha kusini mwa Libya, kabla ya kuwekwa katika gereza moja bovu, ambapo zaidi ya wahamiaji 100 walikuwa wakizuiwa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kila mwaka maelfu ya wahamiaji huvuka bahari ya Mediterranean kuelekea Bara Ulaya

Amesema kwamba, wahamiaji wanaozuiliwa waliambiwa kuwapigia simu familia zao, ambao waliulizwa kutoa fedha ya kikombozi ili waachiwe huru, na baadhi yao wakapigwa wakiwa bado wanazungumza kwenye simu, ili kuwafanya jamaa zao wasikie wakiteswa ili watume haraka fedha hizo.

Ameelezea kuwa ni matendo ya "kutisha" ambapo wahamiaji walilazimishwa kuhimili kula kiwango kidogo mno cha chakula, lakini kwa wale wasioweza kulipia wanauwawa au wanaachwa ili wafe njaa, ripoti hiyo inaongeza.

Haki miliki ya picha Unicef
Image caption Ramani inayoonyesha namna uhamiaji huwa kutoka Bara la Afrika hadi Ulaya

Mfanyikazi mmoja wa IOM nchini Niger, amesema kwamba ripoti ya biashara ya utumwa nchini Libya ni ya hakika, baada ya kuzungumza na wahamiaji waliotoroka kutoka kambi za kuwazuilia wahamiaji.

"Wote walielezea hatari ya kuuzwa walipokuwa wamezuiliwa kwenye viwanja na karakana za magari huko Sabha, aidha na madereva wao au wenyeji wanaowaandikisha wahamiaji kufanya vibarua vya kila siku mjini humo, wengi wao kama wajenzi.

"Baadaye, badala ya kulipwa, wanauzwa kwa wanunuzi wapya."

Baadhi ya wahamiaji, wengi wao kutoka Nigeria, Ghana na Gambians wanalazimishwa kufanya kazi" kama walinzi katika majumba ya kupokea fedha za kikombozi au katika 'soko lenyewe", mfanyikazi huyo wa IOM aliongeza.