Tanzania yaanza kujenga reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro

Rais wa Magufuli leo ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli ya kisasa
Maelezo ya picha,

Rais wa Magufuli leo ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli ya kisasa

Rais wa Tanzania John Magufuli leo hii ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi mkubwa wa reli ya kisasa ya Standard Gauge ambayo hapo baadae itaunganisha nchi za Rwanda na Burundi pia.

Lakini katika awamu hii ya kwanza, ujenzi utakuwa wa reli yenye urefu wa kilomita takribani 300, ambayo itatoka jijini Dar es Salaam na kuishia mkoa wa jirani wa Morogoro.

Ni reli ya kisasa, na ya kwanza Afrika Mashariki na kati itakayokuwa na uwezo wa kupitisha treni zitakazoendeshwa kwa nguvu ya umeme.

Reli hiyo itajengwa kwa awamu ya kwanza na kampuni kutoka nchi mbili, uturuki na Ureno kwa gharama ya takriban dola bilioni 1.2 za Kimarekani.

Reli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba treni yenye kuvuta mabehewa 100 na kubeba mzigo wa mpaka tani 10000 kwa mkupuo sawa na uwezo wa Malori 500 ya mizigo.

Mradi huu utaleta ahueni kwa wasafiri wa Dar es Salaam mpaka Morogoro ambpo wataweza kusafiri kwa mwendo kasi kwa saa 2 na dakika 50 pekee

Rais wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli katika sherehe hizo amesema kuwa Tanzania itanufaika kutokana na Mradi huu kwa maendeleo ya uchumi,

Hivi sasa Serikali ya Tanzania inaelekeza jitihada zake za ujenzi wa reli wa awamu ya pili yenye urefu wa kilometa 336 kutoka Morogoro mpaka Dodoma yalipo makao makuu ya nchi na tayari serikali ya Uturuki imeonyesha nia ya kushirikiana na Tanzania kujenga sehemu hiyo.