Trump amshutumu Bashar Al Assad kama mtu katili

Rais wa Syria Bashar Al Assad

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Rais wa Syria Bashar Al Assad

Rais wa Marekani Donald Trump amemshutumu Rais Bashar Al Assad kama mtu katili na pia ametaka kumalizwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari, akiwa pamoja na Katibu mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya Nchi za Magharibi -NATO- Jens Stoltenberg, Rais Trump amelaani kile alichokiita mauaji ya kikatili ya raia wasio na hatia katika shambulio la wiki iliyopita, ambalo linadaiwa kutumia silaha za kikemikali katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Khan Sheikhoun.

Akiielezea Urusi kuwajibika kwake katika shambulio hilo, Rais huyo wa Marekani amesema ni jambo la kusikitisha.

Rais Trump amesema hana shaka yoyote kwa sababu amefanya jambo lililo sahihi kutoa agizo la kushambuliwa kwa makombora katika kambi ya jeshi la anga ya Shayrat nchini Syria.