Mamilioni ya dola yanaswa Nigeria

Wakuu wa usalama nchini Nigeria wakionyesha zaidi ya dola milioni 40 pesa taslimu

Chanzo cha picha, Economic and Financial Crimes Commission

Maelezo ya picha,

Wakuu wa usalama nchini Nigeria wakionyesha zaidi ya dola milioni 40 pesa taslimu

Wakuu wa usalama nchini Nigeria, wamefichua zaidi ya dola milioni 40 pesa taslimu, iliyo kwenye sarafu ya pesa za Nigeria na ya kimataifa, baada ya msako wa ghafla katika nyumba moja mjini Lagos.

Tume ya kupambana na uhalifu wa uchumi na kifedha (EFCC), imesema kuwa, ilipata "noti nyingi za Marekani, pouni ya Uingereza na nyingine za naira, kwenye mifuko iliyokuwa imefungwa barabara, ndani ya nyumba moja yenye vyumba vinne vya kulala.

Inasema kwamba wapelelezi waliingia kwa nguvu ndani ya maskani hiyo na kunasa dola milioni 43 nukta 4, Pauni Milioni 27 na laki 8 na Naira milioni 23 nukta 2, taslimu.

Chanzo cha picha, Economic and Financial Crimes Commiss

Maelezo ya picha,

Baada ya upekuzi zaidi, walipata mabunda mengine ya pesa ndani ya kabati la nguo

Aida taarifa zinasema kuwa, baada ya kupekuwa zaidi mojawepo nya vyumba hivyo, walipata pesa zaidi ndani ya kabati la nguo.

Inasemekana kuwa fedha hizo zinaaminika kupatikana kupitia njia haramu.

Tume ya EFCC, inasema kuwa, mfichuzi wa kashfa hiyo, aliwajulisha wapelelezi kuhusiana na mienendo iliyojaa shaka kuhusiana na mabegi yaliyokuwa yakiletwa na kutolewa kwenye nyumba hiyo mara kwa mara:

Duru zaidi kutoka kwa mmoja wa wanaoishi karibu na hapo, zinafichua kuwa, "mwanamke mmoja amekuwa akionekana katika jumba hili mara kwa mara akiwa na mabegi yenye maandishi Ghana Must Go. Alikuwa akionekana mwenye uchovu, mavazi machafu na mwenye wasiwasi mwingi, lakini urembo wake haukuwa ukiendeshana na mavazi hayo, pengine kujifanya ili asitambuliwe." alisema jirani huyo.

Chanzo cha picha, Economic and Financial Crimes Commiss

Maelezo ya picha,

Haya ndio majengo ambayo mabunda hayo ya pesa yalipatikana

Taarifa nyingine zinasema kuwa, maafisa wa usalama waliwahoji walinzi katika eneo hilo na wakasema kuwa hakuna mtu aliyekuwa akiishi katika jumba hilo.