Bashar Al Asaad akana matumizi ya kemikali Syria

Bashar Al Asaad amekuwa madarakani tokea mwaka 2000
Maelezo ya picha,

Bashar Al Asaad amekuwa madarakani tokea mwaka 2000

Rais wa Syria Bashar Al Asaad amekanusha ripoti kwamba wanajeshi wake walitekeleza shambulizi wakitumia silaha za kemikali mapema mwezi huu.

Kiongozi huyo amesema taarifa hizo hazina msingi wowote.

Shambulio hilo liliwaua raia wengi na kupelekea Marekani kushambulia kambi ya jeshi la Syria.

Siku tisa zilizopita dunia ilishangazwa na picha za watoto waliokua na shida ya kupumua baada ya kutokea shambulio la silaha za kemikali eneo la Khan Sheikhoun nchini Syria linalodhibitiwa na waasi.

Picha nyingine ziliwaonyesha watoto na watu wazima waliokufa kutokana na gesi hiyo.

Maelezo ya picha,

Watu wengi walionekana kushindwa kupumua baada ya shambulizi hilo

Hata hivyo sasa kiongozi wa Syria Bashar Al Asaad amesema huo ni uzushi na kwamba hakuna ukweli wowote.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa kanda na picha zilizokua zinasambazwa ni za uongo, huku akiwataja waokoaji wa Syria wa White Helmet kama magaidi.

Marekani ilijibu kwa kushambulia kambi ya wanahewa wa Syria.

Bashar Al Asaad sasa anasema matukio ya wiki mbili zilizopita yalipangwa na makundi ya kigaidi kwa ushirikiano na Marekani.

Mwaka wa 2013, wachunguzi wa kimataifa walilalamikia Syria kwa kutumia gesi ya sumu dhidi ya raia wake.