Rais Magufuli alaani mauaji ya polisi 8 Tanzania

Rais John Pombe Magufuli
Maelezo ya picha,

Rais John Pombe Magufuli

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na kushutumu mauaji ya polisi wanane wa taifa hilo waliouawa na watu wasiojulikana jioni siku ya Alhamisi.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari wanane hao walikuwa wakitoka kubadilishana doria waliposhambuliwa kwa kupigwa risasi katika eneo la Jaribu mpakani mwa wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.

Walikuwa wakisafiri kwa gari katika barabara ya Dar es Salaam na Lindi.

Magufuli amelaani tendo hilo na matukio yote ya kuwashambulia polisi akisema wanafanya kazi kubwa ya kuwalinda raia.

Ametuma rambirambi kwa jamaa na marafiki walioguswa na vifo hivyo huku akiwataka raia wote kushirikiana katika kukomesha vitendo kama hivyo.

''Nimeshtushwa na nimesikitishwa sana na vifo vya asakari wetu 8 ambao wamepoteza maisha wakiwa wanalitumikia taifa, naungana na familia za marehemu wote, jeshi la polisi na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi ya kuondokewa na vijana wetu shupavu,namuomba mungu atupe myo wa subira ,uvumilivu na ustahimilivu'',alisema rais Magufuli