Wenger: Hatuna hakika kuhusu nafasi nne bora EPL

Arsene Wenger na mshambuliaji wake Alexis Sanchez
Maelezo ya picha,

Arsene Wenger na mshambuliaji wake Alexis Sanchez

Arsenal inakabiliwa na changamoto kubwa kufuzu katika kombe la vilabu bingwa Ulaya kulingana na mkufunzi wa klabu hiyo Arsene Wenger ambaye ameongezea kuwa hakuna kilichobadilika kuhusu hatama yake ya siku zijazo.

Kushindwa kwao kwa 3-0 na Crystal Palace kuliiwacha klabu hiyo ikiwa katika nafasi ya sita ,na ponti saba nyuma ya klabu ya Manchester City iliopo katika nafasi ya nne huku ikiwa imesalia mechi nane pekee.

Wenger ambaye kandarasi yake inakamilika mwisho wa msimu huu ameiongoza Arsenal katika nafasi nne bora za ligi hiyo katika miaka 20 aliyokuwa mkufunzi wake.

Kuhusu timu nne bora, alisema: ''Tunaweza kuwa katika timu nne bora au la''.

Raia huyo wa Ufaransa amepewa ombi la kandarasi ya miaka miwili ijapokuwa hajatangaza iwapo ataendelea au la.

Kushindwa kwao kwa mechi tano kati ya 10 katika mechi za ligi kuu kumewafanya mashabiki wa Arsenal kumtaka Wenger kuondoka katika klabu hiyo.

Alipoulizwa kuhusu hatma yake ya baadaye alisema: kile kitakachoamuliwa na bodi hakinihusu mimi.

''Ninafanya kile nilichoajiriwa kufanya, mchezo mzuri wa timu na kile mashabiki wanachotaka ambacho ni timu iweze kucheza vyema''.

The Gunners watacheza dhidi ya Middlesborough siku ya Jumatatu.

Wenger amekataa kujibu madai kwamba mshambuliaji Alexis Sanchez amepewa kandarasi mpya ya £300,000 kwa wiki.