Marekani ''ilidukua mfumo wa benki wa dunia''

NSA imelaumiwa kwa kukataa kugawana mianya ya usalama na kampuni ya Microsoft
Maelezo ya picha,

NSA imelaumiwa kwa kukataa kugawana mianya ya usalama na kampuni ya Microsoft

Wadukuzi nchini Marekani wamechapisha habari zinazoonyesha kuwa idara ya ujasusi nchini Marekani NSA imekuwa ikichunguza ubadilishanaji wa fedha kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

Habari hizo zinaonyesha kuwa shirika la ujasusi la kitaifa limeweza kupenya programmu ya kutuma pesa ya SWIFT, ambapo serikali inawezeshwa kujua jinsi mamilioni ya dola yanavyowekwa na kutolewa kwenye benki hasa katika Mashariki ya Kati.

Wachanganuzi wa maswala ya usalama wa mitandao, Cybersecurity, wanasema kuwa habari zilizochapishwa zina takwimu zinazoweza kutumiwa na wahalifu kuibia benki.

Nakala hizo zilitolewa na Shadow Brokers, kundi la wadukuzi ambalo awali lilidaiwa kufichua programu za siri.

Iwapo hatua hiyo itabainika kuwa ya ukweli basi inawakilisha ufichuzi mkubwa wa kitengo hicho cha Marekani tangu ule uliofanywa na Edward Snowden 2013.

Katika mtandao wa Twitter, bwana Snowden aliitaja hatua hiyo kuwa ''Mother of All Exploits'' {hatua kubwa zaidi ya utumizi mbaya wa vifaa'',akifananisha na bomu kubwa la Marekani lililodondoshwa nchini Afghanistan.

Wataalam tofauti wamesema kuwa data iliopatikana huenda ni ya kweli lakini taasisi zinazodaiwa kufanya udukuzi huo zimekana habari hizo.

Swift ambayo ina makao yake Ubelgiji ilisema: Hatuna ushahidi wa kusema kuwa kumekuwa na uingiliaji wa mtandao wetu ama hata huduma ya ujumbe.

BBC haiwezi kuthibitisha ukweli wa nakala hizo, na shirika hilo la kijasusi halijatoa tamko lolote kuhusu siri zilizofichuliwa.