Kura ya Maoni Uturuki: Upinzani wapinga matokeo yaliyomuongezea nguvu Erdogan

Wafuasi wa upinzani watokea mitaani mjini Istanbul wakipiga sufuria

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wafuasi wa upinzani walitokea mitaani mjini Istanbul wakipiga sufuria

Chama kikuu cha upinzani Uturuki kimesema kuwa kitapinga matokeo ya kura ya maoni baada ya rais Recep Tayyip Erdogan kushinda kura ya kumuongezea mamlaka.

Chama cha Republican People Party (CHP) kinapinga uhalali wa matokeo hayo yaliyokaribiana sana na kusema kulikuwa na kasoro nyingi.

Upande wa rais Recep Tayyip Erdogan uliokuwa unatetea kuwe na rais mwenye mamlaka makuu ulipata ushindi kwa kuzoa asilimia 51 ya kura zilizopigwa.

Ushindi huo ulipokewa kwa sherehe na pia maandamano nchini humo.

CHP kimekataa kukubali matokeo ya ushindi wa Ndio na kimeitisha kurudiwa kwa kura asilimia 60, wakikashifu uamuzi wa kupitisha kura ambazo hazikupigwa muhuri kama halali hadi pale zitakapokataliwa.

Mitatu kati ya miji mikubwa nchini Uturuki - Istanbul, Ankara and Izmir - yote zilipiga kura ya La wakipinga marekebisho katika katiba.

Wafuasi wa upinzani wametokea mitaani mjini Istanbul wakipiga sufuria - utamaduni wa tangu jadi wa maandamano - huku wakiandamana wakipiga kelele.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Wafuasi wa bwana Erdogan walisherehekea wakipeperusha bendera

Wakati huo huo, wafuasi wa Bw Erdogan walisherehekea wakipeperusha bendera, huku rais wao akiwasifu kwa "uamuzi wao wa kihistoria" ambao utaendelea kumuweka madarakani hadi 2029.

Huku asilimia 99.97 ya kura zikiwa zimehesabiwa, kampeni ya Ndio ilishinda kwa asilimia 51.41 ya kura zilizopigwa, huku La ikichukua asilimia 48.59.

Kando na hayo, watu watatu walipigwa risasi na kufa nje ya kituo cha kupigia kura katika mkoa wa kusini mashariki mwa Diyarbakir, katika mzozo kuhusu upigaji kura.

Akiongea kuhusu matokeo ya Jumapili, Tume ya Ulaya ilitoa taarifa ikimshawishi bwana Erdogan kuheshimu ukaribu wa kura na kutafuta njia mwafaka ya upatanisho ikikusudiwa athari kwa marekebisho ya katiba.

Chanzo cha picha, ADAM BERRY

Maelezo ya picha,

Msukumo wa rais Recep Tayyip Erdogan kuwepo kwa rais mwenye mamlaka makuu ilishinda na zaidi ya kura asilimia 51.

Gani jipya ndani ya katiba mpya?

Rasimu inasema kuwa uchaguzi ujao wa rais na bunge utakuwa tarehe 3 Novemba 2019.

Rais atashikilia usukani kwa miaka mitano, na hatapitisha vipindi viwili.

  • Rais ataweza kuchagua maafisa wa juu serikalini wakiwemo mawaziri.
  • Ataweza kuwapa kazi naibu rais mmoja au marais kadhaa.
  • Nafasi ya waziri mkuu ambayo kwa sasa inashikiliwa na Binali Yildirim, itafutwa.
  • Rais atakuwa na nguvu za kuingilia kati mahakama, ambayo Bw Erdogan ameikashifu kwa kuathiriwa na Fethullah Gulen, mhubiri kutoka Pennsylvania anayemlaumu kwa mapinduzi yaliyofeli Julai.
  • Rais ataamua iwapo ataweka hali ya hatari nchini au la.

Chanzo cha picha, BURAK KARA/GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Maelfu ya watu wameshikwa na takribran watu 100,000 wamefutwa au kuachishwa kazi kwa muda tangu jaribio la mapinduzi Julai mwaka uliopita.

Serikali ya wakati wa hatari

Waturuki wengi tayari wanahofia utawala wa kimabavu nchini mwao, ambapo maelfu ya watu wameshikwa na takribran watu 100,000 wamefutwa au kuachishwa kazi kwa muda tangu jaribio la mapinduzi Julai mwaka uliopita.

Kampeni zilifanywa wakati wa hali ya hatari baada ya jaribio la mapinduzi kufeli.

Bw Erdogan alichukua usukani kama rais mwaka wa 2014 baada ya kuhudumu kwa zaidi ya muongo mmoja kama waziri mkuu.