Wapalestina waliofungwa jela Israel waanza kususia chakula

Barghouti (aliye pigwa picha kwa bango) ni kati ya Wapalestina 7,000 waliokizuizini katika jela za Israeli.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Barghouti (aliyepigwa picha kwa bango) ni kati ya Wapalestina 7,000 walio vizuizini katika jela za Israeli.

Mamia ya Wapalestina waliofungwa jela Israel wameanza kususia chakula wakilalamikia hali duni ya mazingira yao.

Hatua hiyo inaongozwa na Marwan Barghouti, kiongozi wa Palestina aliyehukumiwa kufungwa jela maisha na Israel kwa makosa matano ya mauaji.

Barghouti, ambaye ana ushawishi mkubwa katika kikundi cha rais wa Palestina Mahmoud Abbas cha Fatah, anasemekana kuwa na nafasi kubwa ya kumrithi bwana Abbas.

Inahofiwa kuwa maandamano hayo yanaweza kuchochea ghasia katika eneo linalokaliwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi

Kulingana na huduma ya magereza ya Israel, Wapalestina 1,187 walio ndani ya jela wanaunga mgomo huo ambao umelingana na maadhimisho ya Siku ya Wafungwa wa Palestina.

Suala la Wapalestina kufungwa katika jela za Israel limekuwa suala la mvutano kati ya pande hizo mbili.

Wapalestina wamezingatia waliowekwa kizuizini kama wafungwa wa kisiasa, wengi ambao wamehukumiwa kwa mashambulizi dhidi ya Israel miongoni mwa makosa mengine.

Wengine wameshikwa kwa kile kilichotajwa kama Kuzuiliwa kwa Kiutawala, sheria ambayo inakubali washukiwa kuzuiwa bila kusomewa mashtaka kwa muda wa miezi sita.

Kuna takriban Wapalestina 7,000 waliowekwa vizuizini katika jela za Israel kufikia mwisho wa mwaka jana, kulingana na vikundi vya wafungwa wa Palestina.