Mkenya Sarah Ikumu ashangaza kwa kipaji Britain's Got Talent Uingereza

Bi Sarah Ikumu

Chanzo cha picha, Sarah Ikumu/ Instagram

Kijana Mwingereza ambaye wazazi wake Wakenya amevuma sana mtandaoni baada ya kusisimua kwa wimbo katika shindano la vipaji katika sanaa Uingereza la Britain's Got Talent Jumamosi.

Sarah Ikumu, 16, aliyezaliwa Uingereza, aliwashangaza wengi katika kipindi cha vipaji cha Britain's Got Talent, alipoimba wimbo wa And I'm Telling You ambao unadaiwa kuwa mgumu sana kuuimbwa ipasavyo.

Wimbo huo wake Jennifer Holliday ulitumiwa kwenye filamu ya Dreamgirls iliyotolewa mwaka 2006.

Uimbaji wa Sarah uliwaacha waliohudhuria mashindano hayo wakiwa wameduwaa huku wote wakisimama na kumshangilia.

Kilele cha uimbaji wake kikifika pale mmoja wa majaji ambaye anajulikana kuwa mgumu kufurahisha, Simon Cowell, alipobonyeza kengele ya dhahabu ambayo humpeleka mshiriki moja kwa moja hadi nusu fainali ya mashindano hayo.

Sarah ambaye anasomea Milton Keynes alianza kuimba akiwa na miaka mitano huku akishiriki kwa mashindano kadha ya nyimbo.

Lakini hili ndilo shindano la kwanza ambalo anasema kuwa ni ndoto ambayo imetimia, mwanzo pale Jaji Simon alipompongeza kwa talanta yake akimuambia "lilikuwa jambo la kushangaza kwa mtu rika lake kusimama mbele ya watu akiwa na hofu na kuelekea kuimba wimbo ni kama ameutunga mwenyewe".

Mwimbaji mashuhuri ambaye pia ni jaji Alesha Dixon alimwambia Sara kuwa "'hakubaliwi' kuwa na talanta kama hii katika umri wake"

Majaji wengine wawili wakiwemo David Williams, Amanda Holden pia walimmiminia pongezi.

Mitandao ya kijamii ilifurika watu wakimsifu.