Ethiopia yakataa wachunguzi wa kigeni

Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn

Ethiopia imepuuza pendekezo la Umoja wa mataifa na Muungano wa EU wa kutaka wachunguzi wa kimataifa kuingia nchini humo na kuchunguza vifo vya mamia ya watu wanaodaiwa kuuwawa kufuatia miezi kadhaa ya maandamano ya kuipinga serikali.

Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn ameiambia BBC kuwa tume ya kitaifa ya haki za Kibinadamu tayari inachunguza visa hivyo. Mapema mwezi huu mjumbe maalum wa Muungano wa EU kuhusu haki za kibinadamu aliitaka Ethiopia kushirikiana na Umoja wa mataifa kuhusu suala hilo.

Bunge la nchi hiyo hivi majuzi liliongeza muda wa hali ya hatari iliyotangazwa mwezi Oktoba mwaka kwa miezi minne zaidi.

Akizungumza na BBC Waziri mkuu huyo ametetea hatua ya serikali yake kuongezea muda tangazo la hali ya hatari iliyotangazwa mwezi Oktoba mwaka jana,akidai hali hiyo ilihitajika ili kuweza kukabiliana na baadhi ya watu ambao bado wana nia ya kuleta ghasia.

Kuhusu uchunguzi wa vifo vya mamia ya Watu waziri Desalegn amesema ni lazima haki ipatikane kwa sababu kuna nia ya kushughulikia hilo ndani ya Serikali. Amesema uchunguzi umefanywa na matokeo yake yatawekwa wazi.