Uturuki: Trump ampigia simu Erdogan kumpongeza

Nje ya makao makuu ya chama cha AK 16 Aprilu 2017 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wafuasi wa Bw Erdogan walisherehekea matokeo mjini Istanbul

Rais wa Marekani Donald Trump amempigia simu Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na kumpongeza kufuatia ushindi wake kwenye kura ya maoni iliyoandaliwa Jumapili kumuongezea mamlaka.

Rais huyo pia alimpongeza Erdogan kwa kuunga mkono shambulio la Marekani la makombora katika uwanja wa ndege za kivita za Syria mnamo 7 Aprili.

Matokeo yaliyotangazwa baadaye Jumatatu yalionesha asilimia 51.4 ya waliopiga kura waliunga mkono marekebisho ya katiba yaliyokuwa yamependekezwa.

Bw Erdogan alipuuzilia mbali shutuma kutoka kwa waangalizi wa kimataifa kwamba alipendelewa na "kampeni ambazo ziliegemea upande mmoja".

"Mnaifahamu nafasi yenu," aliwaambia waangalizi.

Ushindi wa Bw Erdogan, kwa kura chache, uliidhinishwa na tume ya uchaguzi ya Uturuki licha ya kuwepo madai ya udanganyifu ambayo yaliibuliwa na upinzani.

Hayo yakijiri, Uturuki imeidhinisha kuongezwa kwa hali ya hatari kwa miezi mitatu.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wapiga kura walikuwa wanaamua 'Ndio' au 'La' kuunga mkono au kupinga marekebisho hayo

Hali ya hatari, iliyotangazwa baada ya jaribio la mapinduzi ya serikali lililofeli Julai mwaka jana, ingemalizika katika kipindi cha siku mbili zijazo.

Gani jipya ndani ya katiba mpya?

  • Rasimu inasema kuwa uchaguzi ujao wa rais na bunge utakuwa tarehe 3 Novemba 2019.
  • Rais atashikilia usukani kwa miaka mitano, na hatapitisha vipindi viwili.
  • Rais ataweza kuchagua maafisa wa juu serikalini wakiwemo mawaziri.
  • Ataweza kuwapa kazi naibu rais mmoja au marais kadhaa.
  • Nafasi ya waziri mkuu ambayo kwa sasa inashikiliwa na Binali Yildirim, itafutwa.
  • Rais atakuwa na nguvu za kuingilia kati mahakama, ambayo Bw Erdogan ameikashifu kwa kuathiriwa na Fethullah Gulen, mhubiri kutoka Pennsylvania anayemlaumu kwa mapinduzi yaliyofeli Julai.
  • Rais ataamua iwapo ataweka hali ya hatari nchini au la.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii