May aitisha uchaguzi wa mapema Uingereza 8 Juni

Theresa May

Chanzo cha picha, PA

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ameitisha uchaguzi mkuu wa mapema nchini humo ambao utafanyika tarehe 8 Juni.

Ameliomba Bunge la Commons kuunga mkono pendekezo lake hilo hapo kesho, ambapo ndipo liidhinishwe, litahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge.

Amesema Uingereza inahitaji mazingira ya uhakika na uthabiti kufuatia hatua ya taifa hilo kupiga kura kujiondoa kutoka kwa Umoja wa Ulaya mwaka jana.

Bi May amesema: "Nchi unaungana pamoja, lakini Westminster (Wabunge) hawaungani pamoja."

Uchaguzi mkuu ulikuwa umepangiwa kufanyika 2020.

Bi May alikuwa amesisitiza kwamba hataitisha uchaguzi wa mapema.

Lakini akitetea msimamo wake huo mpya, amesema: "Nimeamua kwamba njia pekee ya kuhakikisha uthabiti na usalama miaka ijayo ni kuandaa uchaguzi huu."