Weetabix kununuliwa na kampuni ya Post Holdings ya Marekani

Weetabix - Iliyotengenezewa Uingereza tangu 1932 - iliuzwa January na kampuni ya Uchina Bright Food, ambayo ilikuwa imenunua aslimia 60 ya kampuni hiyo 2012.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Weetabix imekuwa ikitengenezewa Uingereza tangu 1932

Kampuni ya Uingereza ya vyakula vya nafaka vya Weetabix inatarajiwa kununuliwa na kampuni ya Post Holdings ya Marekani kwa takriban dola bilioni 1.8 (£1.4bn), mmiliki wake amethibitisha.

Weetabix, ambayo ni nembo ya vyakula ambavyo vimekuwa vikitengenezewa Uingereza tangu 1932 - iliuzwa Januari kwa kampuni ya Uchina Bright Food, ambayo ilikuwa imenunua asilimia 60 ya kampuni hiyo 2012.

Ununuzi huo wa kampuni ya Bright ulikuwa mkubwa mno kufanywa na kampuni ya Uchina wakati huo.

Lakini kampuni hiyo ilikumbana na wakati mgumu kujenga soko thabiti la bidhaa hiyo nchini China.

Wachina hupendelea kula wali moto kama kiamsha kinywa kuliko nafaka baridi.

Ijapokuwa Weetabix iliongeza mauzo yake Uchina mwaka wa 2016, Uingereza bado yaongoza kwa ununuzi wake.

Kibali cha Kifalme

Kampuni ya Post Holdings ndiyo ya tatu kwa ukubwa katika kampuni za nafaka Marekani na inamiliki bidhaa kama Great Grains, Golden Crisp na Cocoa Pebbles.

Baadhi ya majina makubwa katika utengenezaji wa bidhaa za chakula, ikiwemo kampuni Uingereza ya Associated British Foods na Barilla kutoka Italia, walitajwa kama wanunuzi waliotarajiwa kununua Weetabix.

Weetabix ambayo makao yake makuu ni mji wa Northamptonshire, pia ina kibali cha kifalme na ilimilikiwa na familia moja hadi 2004 ambapo ilinunuliwa na kampuni ya kibinafsi ya Lion Capital.

Kiwanda chake kikuu kinapatikana mjini Kettering kutengeneza biskuti za Weetabix bilioni tatu kila mwaka.

Ndiyo kampuni kubwa zaidi ya vyakula vya nafaka vya kuliwa asubuhi Uingereza na imeajiri watu takriban 2,000.

Bidhaa zake husafirishwa hadi nchi 80 za nje, huku ikiwa na viwanda bara Ulaya, Africa Mashariki na Amerika Kaskazini