Ajali ya boti ziwa Malawi: Mzee anusurika kifo kwa kushikilia mfuko wa unga

Mvuvi atumia kitumbwi

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Ziwa Malawi ni mojawapo ya maziwa makubwa zaidi barani Afrika

Mwanamume mwenye umri wa miaka 67 alinusurika kifo kwa kushikilia mfuko wa unga wa mahindi baada ya mashua aliyokuwa ameiabiri kuzama katika ziwa Malawi.

Graciam Kondowe alikuwa miongoni mwa abiria 54 ambao polisi wanasema walinusurika baada ya boti kupinduka kutokana na hali mbaya ya anga siku ya Jumapili.

Watu tano walikufa maji huku 11 wakiwa bado hawajulikani waliko, kulingana na polisi.

Boti hilo lilikuwa limewabeba waumini waliokuwa wakirejea kutoka sherehe za Pasaka lilipopinduka katika wilaya ya Rumphi, kaskazini mwa Malawi.

Kondowe alieleza kituo cha kibinafsi cha radio, Zodiac, kuwa upepo mkali ulivuma dakika 15 baada yao kuanza safari.

Wafanyakazi waliamua kuirejesha mashua ufuoni lakini boti lilizama kabla hawajafika, alisema.

Kondowe anasema alishikilia kwa nguvu mfuko wa unga wa mahindi ambao ulikuwa kwenye boti, kabla ya kuogelea hadi ufuoni.

Watu nane kati ya 54 walionusurika wanapata matibabu hospitalini baada ya kupata majeraha, alisema afisa wa polisi Denis Banda.

Mwandishi wa habari wa Malawi Yoabu Chakhaza aliiambia BBC ya kuwa wenyeji walitumia mitumbwi kuwaokoa abiria zaidi.

Shughuli za uokoaji zinaendelea ili kuwatafuta watu 11 ambao hawajulikani waliko lakini uwezekano wa kuwapata wakiwa hai ni finyu sana, alisema.

Usafiri wa mashua ni kawaida katika ziwa Malawi lakini ajali za aina hii ni nadra.

Mwaka wa 2012, wahamiaji 47 waliokimbia ukame na migogoro nchini Somalia na Ethiopia walikufa maji katika ziwa hilo baada ya mashua yao kupinduka.