Vibandiko vya njia ya uzazi vyadhuru wanawake Uingereza

Wanawake wengi wanasema kinasababisha uchungu katika njiya ya uzazi
Maelezo ya picha,

Kibandiko cha njiya ya uzazi

Zaidi ya wanawake 800 nchini Uingereza wameshtaki Mamlaka ya huduma ya afya-NHS pamoja na kampuni ya kutengeneza vibandiko, vya njia ya uzazi.

Wanawake hao wamesema vibandiko hivyo ambavyo hutumika zaidi baada ya mwanamke kujifungua mtoto vimewaletea maumivu mengi.

Baadhi wanasema baada ya kuwekwa vibandiko hivyo wameshindwa kutembea na kutekeleza masuala ya unyumba.

Mmoja wa wanawake waliotumia vibandiko hivyo Kate Langley amesema amelazimika kuacha kazi yake ya kuwachunga watoto kutokana na uchungu unaosababishwa na kibandiko alichowekwa.

Ameongeza mama huyo ametembelea hospitali mara 53 na hakuweza kutolewa kibandiko hicho kwa sababu kilikua kimewekwa eneo ambalo hakiwezi kutolewa.

Maelezo ya picha,

Kate Langley aliacha kazi kutokana na madhara ya kibandiko hicho

Vibandiko hivyo hutengenezwa kwa plastiki ambazo hutengeneza baadhi ya chupa za kuweka vinywaji.

Vinatumika sana kusaidia njia ya uzazi, mimba, na mfuko wa mkojo hasa baada ya kujifungua mtoto kwa njiya ya kawaida.

Kati ya mwaka wa 2007 ma 2017 zaidi ya wanawake 90,000 walitumia vibandiko hivi nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa Mamlaka za huduma ya Afya Uingereza -NHS mwanamke mmoja kati ya 11 hukumbwa na matatizo ya vibandiko hivi.

Wanawake wengi waliozungumza na BBC wamesema wataalamu wa afya hawakuwaarifu kuhusu madhara ya vibandiko hivyo.

Hii ndio maana wameamua kushtaki NHS na kampuni ya dawa ya Johnson & Johnson inayotengeneza vibandiko hivyo.