Zimbabwe yasherehekea uhuru wake

Kiongozi huyu wa miaka 93 ameongoza Zimbabwe tangu kupata uhuru mwaka wa 1980

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe anatarajiwa kuongoza taifa hilo kuadhimisha miaka 37 ya uhuru kutoka kwa Uingereza.

Mugabe wa miaka 93 amepangiwa kuhutubia taifa wakati nchi hiyo ikikumbwa na uhaba wa fedha.

Wizara ya elimu ilikubali mifugo kutumiwa kulipa karo au mzazi kufanya ajira shuleni.

Katibu Mkuu katika wizara ya elimu Sylvia Utete-masango ameambia gazeti la serikali kwamba waalimu hawafai kuwafukuza wanafunzi shuleni kwa sababu ya karo.

Aliongeza bi Sylvia Utete-Masango kwamba wazazi ambao hawana karo wanaweza kutoa mifugo kama karo. Hii ni hasa kwa wazazi katika maeneo ya vijijini. Wale wazazi walioko maeneo ya mijini wanaweza kujitolea kufanya ajira shuleni kugharamia karo ya watoto wao.

Serikali ya Zimbabwe, imeanzisha hati za dhamana kama sarafu, kuchukua nafasi ya dola ya Marekani ambayo imekua inatumika.

Sarafu rasmi ya Zimbabwe iliondolewa baada ya kukumbwa na mfumuko wa bei.

Licha ya matatizo ya kiuchumi, Rais Mugabe anatarajiwa kuelezea mafanikio ya taifa lake tangu kupata uhuru.

Bwana Mugabe ameongoza Zimbabwe tangu kupata uhuru wake mwaka wa 1980. Viongozi wa dunia akiwemo Rais wa Urusi Vladmir Putin na Malkia wa Uingereza wametuma salamu za heri njema kwa Zimbabwe wakati wa kusherekea uhuru wake.