Marine Le Pen kuzuia wahamiaji halali Ufaransa

Mgombea huyu ameapa kumaliza uhamiaji haramu Ufaransa

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Marine Le Pen mgombea Urais Ufaransa

Mmoja wa wagombea wakuu katika uchaguzi wa Urais nchini Ufaransa, Marine le Pen amesema atazuia wahamiaji halali kuingia nchini humo.

Kiongozi huyo wa chama cha National Front amehutubia mkutano wa hadhara na kusema lazima atazima kile alichokitaja kama mrundiko wa wahamiaji wote hata walio halali.

Kura ya maoni inaonyesha Marine le Pen na mgombea wa mrengo wa kati Emmanuel Macron wakiongoza katika awamu ya kwanza ya uchaguzi huo.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Emmanuel Macron mgombea Urais Ufaransa

Bwana Macron kwa upande wake amewaonya wapiga kura dhidi ya kumuunga mkono mgombea wa kushoto Jean-Luc Me'lenchon.

Wadadisi wanasema bi Le Pen na Macron watachuana kwenye awamu ya pili na huenda Macron akanyakua ushindi.

Kuna wagombea 11 wa Urais na thuluthi moja ya raia wa Ufaransa hawajaamua nani wataunga mkono. Kura ya kumchagua Rais mpya inafanyika Jumapili ya Aprili 24.