Democrat wapanga kushinda chama cha Trump Georgia

Jon Ossoff anamiliki kampuni ya makala za video ya Insight TWI

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Jon Ossoff anamiliki kampuni ya makala za video ya Insight TWI

Mgombea ubunge wa chama cha Democratic anapania kuandikisha ushindi wa kushangaza katika eneo la Atlanta katika jimbo la Georgia nchini Marekani kwenye uchaguzi ambao unatazamwa na wengi kama mtihani kwa Rais Donald Trump.

Jimbo hilo limekuwa chini ya chama cha Republican lakini mgombea wa Democratic Jon Ossoff ameimarika sana katika kura za maoni.

Amekuwa akiendesha kampeni kali iliyopewa jina Make Trump Furious, maana yake Mfanyeni Trump Akasirike.

Kiti cha ubunge cha Atlanta katika jimbo hilo kilibaki wazi baada ya mbunge Tom Price kujiuzulu na kujiunga na serikali ya Trump.

Kuna wagombea 18, wakiwemo 11 wa Republican jambo ambalo linatishia kugawanya kura za chama hicho cha Rais Donald Trump.

Rais Donald Trump ameonekana kufuatilia uchaguzi huo na mara kadha ameandika kwenye Twitter akiwahimiza wanachama wa Republican kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Wilaya hiyo ya Atlanta imewakilishwa na wanasiasa wa Republican tangu mwaka 1979, lakini wakati huu wapinzani wao wana nafasi nzuri.

Chama cha Republican kilinusurika aibu wiki iliyopita baada ya kufanikiwa kutetea ubunge katika jimbo la kihafidhina Kansas, wadhifa ulioachwa wazi na Mike Pompeo aliyeteuliwa na Trump kuongoza CIA.

Uchaguzi utafanyika vipi?

Kuna wagombea 18, wakiwemo 11 wa Republican na watano wa Democratic.

Ikitokea kukosekane mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, wawili walioongoza watashiriki uchaguzi wa marudio tarehe 20 Juni.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Jack Miller, 15, akimpigia debe mgombea wa Republican Karen Handel

Matokeo yatamwathiri Trump?

Iwapo Democrat watapata ushindi wa moja kwa moja Jumanne, inaweza kuwa aibu kuu kwa Rais Trump.

Hilo linaweza kuwachochea wabunge wengine zaidi wa Republican kujitenga na Bw Trump katika ya uchaguzi wa katikati ya muhula mwaka 2018.

Democrat wanatarajia kufaidi kutokana na kushuka kwa umaarufu wa Rais Trump, ambaye kiwango chake cha umaarufu kwa sasa kimefikia 40% kwa mujibu wa Gallup.

Chanzo cha picha, Twitter

Maelezo ya picha,

Trump amewahimiza wafuasi wa Republican kujitokeza kupiga kura