Watatu wauawa kisa cha ubaguzi wa rangi Marekani

Polisi walifunga barabara karibu na eneo la tukio Haki miliki ya picha Fresno County Sheriff
Image caption Polisi walifunga barabara karibu na eneo la tukio

Wazungu watatu waliuawa na mwingine kujeruhiwa vibaya baada ya mtu mweusi mwenye silaha kuanza kufyatulia watu risasi eneo la Fresno, California nchini Marekani, polisi wamesema.

Mkuu wa polisi Jerry Dyer amesema Kori Ali Muhammad alifyatua jumla ya risasi 16 katika muda wa dakika 90 wakati wa shambulio hilo Jumanne.

Alikuwa akisema: Mungu ni Mkubwa kwa Kiarabu alipokuwa akikamatwa na polisi.

Maafisa hata hivyo wanaamini kisa hicho kilikuwa cha chuki za ubaguzi wa rangi na si ugaidi.

Bw Muhammad, 39, alikuwa pia anasakwa kuhusiana na mauaji ya mlinzi nje ya hoteli moja mjini Fresno wiki iliyopita.

Mshukiwa huyo alikuwa ameandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba anawachukia sana Wazungu na pia akaandika ujumbe ulioashiria kwamba alikuwa anaipinga serikali.

"Alitaka kuua watu wengi na alitaka kutekeleza hilo. Kilikuwa kisa cha ghafla tu cha ghasia. Ni mtu ambaye hakuwa amechokozwa na alikuwa na nia ya kutekeleza mauaji."

Babake Muhammad baadaye aliambia gazeti la Los Angeles Times kwamba mwanawe aliamini kwamba alikuwa anashiriki vita vinavyoendelea kati ya Wazungu na watu weusi na kwamba aliamini vita vikali vinakaribia.

Bw Muhammad, ambaye alifahamika sana kwa jina la utani kama Yesu Mweusi sasa anakabiliwa na mashtaka manne ya mauaji na mawili ya kukusudia kuua.

Kisa hicho huenda kikafufua tena mjadala kuhusu haki ya raia kumiliki silaha Marekani.

Watu zaidi ya 30,000 huuawa kwa kupigwa risasi nchini humo kila mwaka.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii