Waziri wa zamani ataka waajiri wanyanyasaji kuhasiwa Uganda

Aliyekuwa waziri wa maadilli nchini Uganda Maria Matembe ametaka waajiri wanyanyasaji kuhasiwa Uganda Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Aliyekuwa waziri wa maadilli nchini Uganda Maria Matembe ametaka waajiri wanyanyasaji kuhasiwa Uganda

Waziri wa zamani nchini Uganda ametoa wito wa kuwahasi wanabiashara wa kigeni ambao huwadhulumu wafanyikazi wao wa kike kimapenzi, gazeti linalomilikiwa na serikali, New Vision, limeripoti.

Wito huo uliotolewa na waziri wa zamani wa Maadili Miria Matembe, unajiri baada ya kusikia ushuhuda wa wanawake wawili ambao walisema walidhulumiwa kingono kazini, kulingana na gazeti hilo.

Mwanamke mmoja alisema kwamba alilazimishwa kufanya tendo la ngono na mwajiri wake kwa kipindi cha miaka miwili, huku mwengine akidai kufungiwa ndani ya ofisi ya mwajiri wake na kudhulumiwa huku mwajiri huyo akiwa ameweka bunduki yake kwenye meza, New Vision iliongeza.

Katika hotuba kwa wanahabari iliyopangwa na wanaharakati wanaofanya kampeni dhidi ya dhulma za kimapenzi, Bi Matembe alisema:

" Sikujua kwamba wanawake wetu wanadhalalishwa hadi kiwango hiki na wale wanaoitwa wawekezaji chini ya pua zetu. Kudhalalishwa huku kunawafanya Waganda wasiwe lolote nchini mwao."

Shirika la kutetea haki za kibinadamu lilisema kuwa pendekezo hilo litasaidia wanawake walioathirika kupata haki.

Mmoja wa wanawake hao alisema kuwa aliporipoti kesi hiyo kwa polisi, aliambiwa ni jambo la kawaida kwa mwajiri kumuuliza mfanyikazi kushiriki ngono.