Mahakama kuamua hatima ya Waziri Mkuu Pakistan

Ameshtakiwa kwa ufisadi, baada ya kupatikana anamiliki akaunti za siri nje ya nchi Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Nawaz Sharif Waziri Mkuu wa Pakistan

Mahakama ya Juu nchini Pakistan inatarajiwa kutoa uwamuzi dhidi ya kesi ya ufisadi inayomkabili Waziri Mkuu Nawaz Sharif.

Kumekua na lalama dhidi ya kiongozi huyo baada ya wanawe watatu kugunduliwa wanamiliki akaunti za siri kufuatia ufichuzi wa stakabadhi za Panama.

Bwana Sharif na familia yake wamekanusha kuvunja sheria yeyote na kusema kesi ya sasa imechochewa kisiasa.

Serikali imesema ina imani Mahakama ya Juu itamuondolea lawama Waziri Mkuu. Kesi dhidi ya Waziri Mkuu imevutia hisia tofauti nchini humo pamoja na kutawala taarifa za magazeti.

Mahakama ya Juu ilikubali kumchunguza bwana Sharif baada ya kiongozi wa upinzani Imran Khan kutishia kuongoza maandamano.

Inadaiwa pesa kutoka akaunti hiyo ya siri zilitumiwa kununua nyumba mjini London Uingereza.

Sharrif amesema nyumba hiyo ilinunuliwa kwa njiya halali.

Hata hivyo wakosoaji wake wamesema akaunti hizo za siri zinatumika na Waziri Mkuu na familia yake kuwepa kodi pamoja na kuvukisha fedha zilizopatikana na njiya haramu.

Mahakama ya Juu inaweza kuamrisha uchunguzi zaidi dhidi ya Waziri Mkuu na hata kumuachisha kazi.

Stakabadhi za Panama zilifichuliwa kutoka kwa kampuni ya wanasheria ya Panama Mosaack Fonseca.

Kampuni hiyo imekua ikiwasaidia wanasiasa na wafanyibiashara kuwa na akaunti za siri katika mataifa ya nje hasa visiwa vya mbali. Akaunti hizi hazionyeshi wamiliki wake halisi .

Mada zinazohusiana