Atakayepinga aliyechaguliwa kuongoza NASA ataonekana kuunga mkono serikali iliopo

Viongozi wa muungano wa NASA nchini Kenya wakiwa katika ukumbu wa Bomas Jijini Nairobi
Image caption Viongozi wa muungano wa NASA nchini Kenya wakiwa katika ukumbi wa Bomas Jijini Nairobi

Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA umesema kuwa utamtangaza atakayeshikilia bendera yake ya urais mnamo tarehe 27 mwezi Aprili 2017.

Akizungumza katika mkutano wa kumlaki gavana wa kaunti ya Bomet Isack Ruto kujiunga na muungano huo kama mmoja wa viongozi wakuu wa chama hicho, waziri wa zamani wa maswala ya kigeni ambaye pia ni seneta wa kaunti ya Bungoma Moses Wetangula amesema kuwa kiongozi huyo atatajwa katika mkutano utakaofanyika uwanja wa Uhuru Park uliopo katikati ya jiji la Nairobi.

Amesema kwamba tayari viongozi hao ambao wamekuwa wakikutana kwa takriban siku tatu zilizopita wamepiga hatua ya kumchagua mmoja wao kuongoza muungano huo.

Viongozi wakuu wa muungano wa NASA ni aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga wa chama cha ODM, aliyekuwa wakati mmoja makamu wa rais Kalonzo Musyoka, wa chama cha Wiper, Moses Wetangula wa chama cha Ford Kenya na Issack Ruto wa chama cha mashinani CCM.

Wetangula amesema kuwa kiongozi atakayetangazwa atakuwa amechaguliwa na viongozi wote watano na kwamba hakuna kiongozi atakayekuwa na pingamizi miongoni mwao.

Amesema kwamba wafuasi wa NASA watakaopinga tangazo hilo watachukuliwa kwamba wanaunga mkono chama tawala cha Jubilee.

Image caption Wafuasi wa chama cha ODM katika muungano wa upinzani nchini Kenya NASA

''Tutatoa tangazo kubwa kuhusu kiongozi wetu ifikiapo tarehe 27 na mfuasi yeyote atakayepinga tangazo hilo ataonekana kuwa mfuasi wa chama tawala cha Jubilee ambacho ndio mpinzani wetu mkubwa katika uchaguzi huu'', alisema Wetangula mbele ya wanachama wa muungano huo waliomshangilia kwa vifijo na nderemo.

Kiongozi huyo aliongezea kwamba makubaliano yote ambayo yaliafikiwa hapo awali kati ya viongozi hao yaliangaziwa na kutatuliwa ikiwemo yale ya ugawanaji wa mamlaka.

''Makubaliano yote ambayo yalikuwa yamewekwa awali yameangaziwa na kutatuliwa na sasa tunasubiri kuweka serikali itakayounganisha wote na sio ile inayoongozwa na watu wawili''.

Awali akizungumza katika mkutano huo aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga alisema kuwa chama hicho sasa kitakuwa na baraza kuu kwa jina ''NASA Pentagon'' kufuatia kujiunga kwa Issack Ruto.

Viongozi wote wakuu wa muungano huo walihudhuria mkutano huo katika ukumbi wa Bomas of Kenya Jijini Nairobi.