Chama tawala Kenya chafutilia mbali uteuzi wa wagombea wake

Katibu mkuu wa chama cha Jubilee nchini Kenya Raphael Tuju
Image caption Katibu mkuu wa chama cha Jubilee nchini Kenya Raphael Tuju

Chama tawala cha Jubilee nchini Kenya kimefutilia mbali shughuli za uteuzi wa wagombea wake katika kaunti zote.

Katibu mkuu wa chama hicho Raphael Tuju amesema kuwa chama hicho kitatoa tarehe mpya za uchaguzi siku ya Jumamosi.

Bwana Tuju hapo awali alikuwa amesema kuwa baada ya mazungumzo na viongozi wakuu wa chama hicho ,ilikubaliwa kwamba uchaguzi huo uahirishwe hadi siku nyengine ili kuweka uwazi na usawa.

Uteuzi wa wagombea ulikuwa umesitishwa katika kaunti za Narok, Kajiado, Kericho, Bomet, Uashin Gishu,Trans Nzoia ,Baringo, Nakuru, Elgeyo marakwet, Nandi, Embu, Kiambu, Murang'a, Kirinyaga na Nyeri

Uchaguzi huo ulikabiliwa na visa vya uchomaji wa vifaa vya kupigia kura, mgomo wa wapiga kura huku kukiwa na hofu ya wizi wa kura na vitisho vya kuhamia vyama vyengine.

Katika maeneo mengine, sajili za tume ya kusimamia shughuli za uchaguzi IEBC za 2013 zilitumika na kuwacha kando majina ya wapiga kura waliosajiliwa huku katika maeneo mengine majina ya wagombea hayakuwepo katika masanduku ya kupigia kura.

Wiki iliopita shughuli kama hiyo ilifanyika katika chama cha upinzani cha ODM kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila odinga ambapo kulikuwa na ghasia katika maeneo ya magharibi mwa Kenya.

Kura ya mwaka huu itafanyika miaka 10 baada ya uchaguzi kama huo kusababisha ghasia zililizosababisha vifo vya watu 1000 huku watu nusu miliona wakipoteza makao yao.

Bwana Kenyatta anatafuta kuhifadhi kiti chake kwa awamu ya pili kama mgombea wa urais wa chama cha Jubilee.

Muungano wa upinzani NASA unatumai kumtaja mgombea wake wiki ijayo.