Wanajeshi 100 wa Afghanistan wauawa katika shambulio

Wanajeshi wa fghanistan wakiimarisha ulinzi baada ya wanajeshi wenzao 100 kuuawa katika shambulio la Taleban Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanajeshi wa fghanistan wakiimarisha ulinzi baada ya wanajeshi wenzao 100 kuuawa katika shambulio la Taleban

Maafisa wa serikali ya Afghanistan wanasema kuwa watu waliokuwa wamevalia sare za jeshi wamewaua zaidi ya wanajeshi 100 katika shambulio la kambi ya kijeshi katika mji wa Kaskazini wa Mazari Sharif.

Msemaji wa jeshi, Nasratullah Jamshidi, ameeleza kuwa watu hao walishambulia wakati wanajeshi walipokuwa wakitoka katika maombi ya Ijumaa katika msikiti kwenye kambi hiyo.

Wanajeshi wengine walilengwa katika duka lililokuwa karibu.

Kundi la Taliban lililodai kuhusika limesema kuwa watu wake walitegua vilipuzi kabla ya kuwaruhusu watu wa kujitolea muhanga kuingia katika kambi hiyo.

Mapigano yaliendelea hadi baadaye mchana na maafisa hao wanasema kuwa wanatarajia idadi ya waliofariki kuongezeka.

Karibu Wataliban kumi walifariki katika makabiliano hayo.

Serikali ya Afghanistan inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi inaendelea kupigana vita vinavyojikokota na Wataliban na makundi mengine ya Waislamu wenye itikadi kali.