United Airlines wachunguza kifo cha sungura mkubwa

A giant rabbit - not Simon Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Sungura wakubwa kama hawa huwa na thamani ya juu

Shirika la ndege la United Airlines linachunguza kifo cha sungura mmoja mkubwa aliyefariki alipokuwa akisafirishwa kwenye moja ya ndege za shirika hilo.

Sungura huyo kwa jina Simon, aliyekuwa na urefu wa sentimeta 90, alipatikana amefariki eneo la kubebea mizigo ndege ilipowasili katika uwanja wa ndege wa O'Hare mjini Chicago kutoka Heathrow, London.

Taarifa katika vyombo vya habari nchini Uingereza zinasema sungura huyo mkubwa alikuwa anasafirishwa kupelekwa kwa mmiliki wake ambaye ni mtu mashuhuri.

United, shirika ambalo limegonga vichwa vya habari kwa mabaya, limesema limesikitishwa sana na kifo cha Simon.

Si jambo nadra sana kwa wanyama kufariki wakisafirishwa kwa kutumia ndege.

Takwimu za Idara ya Uchukuzi ya Marekani zinaonesha mwaka 2015 wanyama 35 walifariki wakisafirishwa kwa ndege za amshirika ya Marekani.

Kumi na wanne walikuwa kwenye shirika la ndege la United Airlines, na wengine tisa wakajeruhiwa.

United walisafirisha wanyama 97,156, hii ikiwa na maana kuwa wanyama 2.37 kwa kila 10,000 ndio walioathiriwa.

Hiki kilikuwa kiwango cha juu zaidi kwa shirika lolote la ndege la Marekani, kwa mujibu wa takwimu hizo.

Taarifa iliyotumwa kwa BBC na United inasema: "Tumesikitishwa sana na habari hizi. Usalama wa wanyama wanaosafiri nasi ni muhimu sana kwa United Airlines na kundi la washirika wetu wa PetSafe.

"Tumewasiliana na mteja na kumpa usaidizi. Tunachunguza kisa hiki."

Haki miliki ya picha Reuters

Gazeti la The Sun limeripoti kwamba Simon alikuwa 'mwana' wa sungura mkubwa sana wa urefu wa mita 1.4 kwa jina Darius.

Mmiliki wake Annette Edwards aliambia gazeti hilo kwamba Simon alikuwa amechunguzwa na daktari wa mifugo saa tatu kabla ya safari hiyo na alikuwa mzima kama kigongo.

Mapema mwezi huu, United walishutumiwa baada ya abiria Dkt David Dao kung'oka meno mawili na kujeruhiwa puani alipotolewa kwa nguvu kutoka kwa moja ya ndege zake.

Machi, United pia walishutumiwa baada ya kuwazuia wasichana wawili waliokuwa wamevalia long'i za kubana kuzuiwa kuabiri ndege yake kutoka Denver kwenda Minneapolis.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii