Facebook kuongezwa masomoni chuo kikuu India

Chuo Kikuu cha Delhi 17 Julai 2006. Haki miliki ya picha AFP/Manpreet Romana
Image caption Facebook huenda ikajumuishwa katika Kiingereza Chuo Kikuu cha Delhi

Kuandika ujumbe na kupakia picha na video limekuwa jambo la kawaida kwa karibu watu 1.8 bilioni wanaotumia mtandao wa kijamii wa Facebook.

Ingawa ujumbe wako wa siasa au salama za heri, pongezi au rambirambi unaweza kupendwa na wenzako, si wengi wanaoweka kuchukulia ujumbe huo kuwa fasihi au kazi ya sanaa.

Lakini sasa Chuo Kikuu cha Delhi (DU) kimechukua msimamo tofauti.

Kinataka kujumuisha kuandika ujumbe wa Facebook kuwa sehemu ya mtalaa wake wa somo la Kiingereza.

Wanafunzi watakuwa wakifunzwa pia jinsi ya kuandika blogu au barua kuu ya kujitambulisha wakati wa kuwasilisha maombi ya kazi.

DU ni miongoni mwa vyuo vikuu bora zaidi nchini India.

Miongoni mwa waliowahi kusomea katika chuo kikuu hicho ni waziri mkuu Narendra Modi na kiongozi wa Burma na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Aung San Suu Kyi.

Mambo hayo yamejumuishwa kwenye mswada wa mtalaa wa Kiingereza ambao unatathminiwa na maprofesa wa DU.

Prof Christel Devadawson, mkuu wa kitivo cha lugha ya Kiingereza aktika chuo kikuu hicho, aliambia BBC kwamba ujumbe kwenye Facebook utatumiwa kama sehemu ya Kozi ya Kuimarisha Ujuzi - ambayo ni sehemu ya somo inayotumiwa kuwapa wanafunzi maarifa na ujuzi wa kuwawezesha kufaa maeneo ya kazi.

Gazeti la Hindustan Times linasema nchini India, mitandao ya kijamii inaweza kumzolea umaarufu mkubwa mwandishi chipukizi au msanii na kumuwezesha kufikia watu wengi au hapa kupata matbaa ya kuchapisha kazi zake.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Facebook hutumiwa an watu 1.8 bilioni

DU si chuo kikuu cha kwanza kuanza kutumia Facebook masomoni.

Nchini Uingereza, Chuo Kikuu cha Salford huwa na shahada ya uzamifu katika mitandao ya kijamii, ambayo imekuwepo tangu 2009.

Walioandaa shahada hiyo wanasema wanaohitimu huandaliwa kuwa watu wa kutumia fikira zao vyema na pia kufana katika tasnia ya Mawasiliano na Uhusiano mwema katika kampuni na mashirika mbalimbali.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii