Binadamu wa kale Homo naledi huenda 'hawakuishi zamani sana'

Naledi Skeleton
Maelezo ya picha,

Homo naledi ana maumbile yanayokaribiana sana na binadamu wa aina ya Homo wa awali

Aina ya binadamu wa kale, ambao walidhaniwa kuwa waliishi miaka zaidi ya milioni tatu iliyopita, hawakuishi muda mrefu sana uliopita, utafiti unaonesha.

Mabaki ya viunzi 15 vya mifupa ambayo inaaminika kuwa ilitoka kwa Homo naledi yalitangazwa mara ya kwanza 2015.

Yalipatikana katika mapango nchini Afrika Kusini na kundi la wataalamu walioongozwa na Lee Berger kutoka Chuo Kikuu cha Wits.

Kwenye mahojiano, Burger sasa anasema huenda mabaki hayo ya mifupa ni ya binadamu walioishi miaka 200,000 hadi 300,000 iliyopita.

Ingawa kwa maumbile yake, viumbe hao wanafanana sana na binadamu wa sasa kwa baadhi ya maumbile, kuna baadhi ya maumbile ya Homo naledi ambayo ni ya binadamu walioishi zamani sana - pengine miaka milioni mbili na zaidi.

"Wanaonekana kuwa aina ya kale kidogo ya binadamu wa sasa - Homo. Inaonekana wana uhusiano fulani na Homo erectus wa zamani au Homo habilis, Homo rudolfensis," alisema mwenzake Prof Berger, John Hawks, kutoka Chuo Kikuu cha Wisconsin.

Ingawa baadhi ya wataalamu wanasema huenda naledi waliishi muda ambao si zamani sana, mwaka 2015, Prof Berger aliambia BBC kwamba huenda mabaki hayo ni ya zaidi ya miaka milioni tatu iliyopita.

Teknolojia ya kukadiria umri wa vitu vya kale inaonesha huenda Homo naledi waliishi kwa pamoja na binadamu waliokaribiana sana na binadamu wa sasa wa Homo sapiens.

Prof Hawks aliambia BBC kwamba: "Wamo katika enzi moja na Neanderthal wa Ulaya, Denisovans wa Asia, na katika enzi moja na binadamu wa kale Afrika."

Mabaki hayo ya naledi yaligunduliwa 2013 ndani ya mapango ya Rising Star.

Prof Berger alisema ishara zilionesha mifupa hiyo iliwekwa kwenye mapango hayo makusudi, labda kwa kipindi kirefu.

Wazo hilo lilizua mjadala kwamba huenda Homo naledi walikuwa na uwezo wa kuwa na itikadi.

Hilo lilipingwa vikali kwamba kuwa na itikadi ni jambo ambalo wengi huamini ni sifa za binadamu wa sasa pekee.

Prof Hawks anasema kundi lake sasa linafanya upelelezi katika mapango ya pili.