Wasifu wa Raila Odinga, kiongozi wa upinzani Kenya

Bw Odinga

Chanzo cha picha, AFP/GETTY

Raila Amolo Odinga alizaliwa Januari tarehe 7 mwaka 1945 Magharibi mwa Kenya katika mkoa wa Nyanza.

Bw Odinga, anayejulikana kwa wafuasi wake kama "Agwambo" kumaanisha mwenyekiti au mtu wa kushangaza kwa lugha yake asili ya Dholuo, ni kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM). Ni kawaida kuwasikia wafuasi wake pia wakimuita 'Baba'.

Aliwahi kuhudumu kama waziri mkuu wa kwanza wa Kenya, wadhifa ulioundwa kufuatia Mkataba wa Kitaifa ulioafikiwa kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008, ambapo aligawana mamlaka na Rais Mwai Kibaki.

Bw Odinga, mwenye umri wa miaka 72 kwa sasa amekuwa miongoni mwa viongozi watano wanaojiita Pentagon ambao wanaongoza muungano wa umoja wa vyama vya upinzani, National Super Alliance (NASA).

Kwenye muungano huo, anashirikiana na Bw Kalonzo Musyoka (makamu wa rais wa zamani na kiongozi wa chama cha Wiper Democratic Movement -WDM), Bw Musalia Mudavadi (makamu wa rais wa zamani na kiongozi wa chama cha Amani National Congress - ANC), Bw Moses Wetangula (kiongozi wa chama cha Forum for Restoration of Democracy Kenya - Ford Kenya) na Bw Isaac Ruto (kiongozi wa Chama cha Mashinani - CCM).

Kama hayati babake, Jaramogi Oginga Odinga, Raila aliishi kukamatwa na kuachiliwa mara kwa mara tangu mwaka 1982 hadi 1991 kwa harakati zake za kupigania mageuzi wakati wa muhula wa pili wa utawala wa rais Daniel arap Moi.

Kufuatia kuidhinishwa kwa katiba mpya, mwezi Agosti, mwaka 2010, amekuwa akisema kwenye kampeni zake kuwa nia yake ni kuleta mageuzi ya kisiasa na pia kumaliza ufisadi.

Bw Odinga ni mwanasiasa anayesifika sana kwa ushawishi wake kisiasa na amekuwa katika msitari wa mbele kuunda vyama vya miungano na wanasiasa ambao ni mahasimu wake.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 1997 ambapo Raila alishikilia nafasi ya tatu, kufuatia kuundwa kwa muungano wa chama chake (NDP) na chama cha rais wa zamani Daniel moi (KANU), aliteuliwa kama waziri wa kawi katika serikali ya muhula wa mwisho wa Moi.

Chanzo cha picha, AFP/GETTY

Maelezo ya picha,

Bw Odinga amekuwa akiikosoa serikali ya Rais Kenyatta akiwa na Bw Musyoka (Kushoto) na Bw Wetangula

Mwaka 2002, baada ya Moi kumuunga mkono uhuru Kenyatta, kama mrithi wake, Raila na maafisa wengine wa KANU ikiwemo Kalonzo Musyoka na wafuasi wengine, walipinga ungwaji mkono wa Kenyatta kugombea Urais.

Waliungana na kiongozi wa upinzani Mwai Kibaki na na kuunda muungano wa National Rainbow Coalition (Narc) ambao baadaye ulishinda uchaguzi wa mwaka 2002.

Raila aliungana na Rais Mwai Kibaki kuunda serikali ya Muungano ya NARC baada ya kumuondoa mamlakani rais mstaafu Daniel Moi.

Mwaka 2005 aliungana na Uhuru Kenyatta aliyekuwa kama kiongozi rasmi wa upinzani, ili kushinda kura ya maoni kuhusu rasimu ya katiba chini ya serikali ya Rais Kibaki .

Wakati Kibaki alipomfuta kazi na washirika wake, aliunda chama cha ODM ambacho kilipiga kura ya 'La' dhidi ya rasimu ya katiba mpya ambayo ilishindwa mwaka 2005.

Aliongoza kampeni mwaka 2007 na kwa shingo upande kukubali ushindi wa rais Kibaki Katika uchaguzi uliokumbwa na utata, ghasia na mauaji.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Bw Odinga alifungwa jela miaka ya 1980

Lakini hatimaye alilazimika kujiunga na Kibaki katika serikali ya Muungano.

Desemba mwaka 2012, Raila alilazimika kupiga moyo konde na kurudiana na Kalonzo Musyoka chini ya muungano wa CORD, kwani daima husema katika siasa, hakuna maadui wa kudumu.

Raila anaamini kuwa Wakenya wanastahili kuhudumiwa vyema zaidi kuliko ahadi wanazopewa na kwamba chini ya utawala wake.

Raila anaahidi kuleta mageuzi na kuhakikisha uongozi bora.

Amekuwa akiahidi kuwa serikali yake itawekeza katika viwanda vya kisasa, mabohari pamoja na vituo vya teknolojia ya mawasiliano katika maeneo ya kuvulia, ushirikiano na sekta ya kibinafsi ili kuimarisha kilimo.

Kwa miaka miwili, pamoja na wanasiasa wengine akiwemo Bw Musyoka na Bw Wetangula, walikuwa wanaishinikiza serikali kufanya mazungumzo na upinzani kuhusu mwelekeo wa nchi.

Baadaye, watatu hao walianzisha kampeni ya kisiasa iliyofahamika kama Okoa Kenya Movement ambapo waliandaa mikutano na maandamano ya kuipinga serikali.

Aidha, walitumia kampeni hiyo kushinikiza mageuzi katika Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC), hatua iliyopelekea kuondolewa kwa aliyekuwa mwenyekiti Ahmed Isaack Hassan.

Agosti 2017, uchaguzi ulipofanyika, tume ya uchaguzi ilitangazwa kwamba alikuwa ameshindwa na Rais Kenyatta.

Alipinga matokeo hayo Mahakama ya Juu na uchaguzi huo ukafutiliwa mbali na uchaguzi mpya kuandaliwa tarehe 26 Oktoba.

Lakini Bw Odinga alisusia uchaguzi huo akisisitiza wkamba mageuzi yalihitajika katika tume ya uchaguzi kabla ya uchaguzi huru na wa haki kufanyika.

Mahakama ya Juu ilipoidhinisha kuchaguliwa kwa Bw Kenyatta na baadaye akaapishwa tarehe 28 Novemba, Bw Odinga alisema kamwe kwamba hatamtambua kama kiongozi aliyechaguliwa na wananchi Kenya.