Ajuza aliyekataliwa na benki kwa kuwa mzee sana Mexico

María Félix Nava, ana miaka 116 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption María Félix Nava ni miongoni mwa binadamu wazee zaidi kwa sasa duniani

Benki moja nchini Mexico hatimaye imesema itamfungulia akaunti ya benki mwanamke wa umri wa miaka 116 ambaye awali alikuwa amekataliwa kwa sababu ya kuwa mzee sana.

Citibanamex ilikuwa imelaumu hitilafu kwenye mfumo wake wa benki ambayo ilizuia maafisa wake kumfungulia akaunti.

Hatua hiyo ya awali ilikuwa imemwacha María Félix Nava akiwa hana njia ya kupokea marupurupu ya kujikimu kimaisha.

Baada ya taarifa kuhusu kisa hicho kuangaziwa na vyombo vya habari

Guadalajara, mmoja wa viongozi wa benki hiyo alijitokeza na akawasilisha hundi yeye binafsi kwa mwanamke huyo.

Sheria kuhusu uwazi hutaka marupurupu yote yalipwe kwa akaunti za benki za mnufaika.

Bi Félix alikaa miezi mitatu bila kupokea marupurupu baada ya kuzuiwa kufungua akaunti ya benki na tawi la benki ya Citinamex.

"Waliniambia umri wa juu zaidi ni miaka 110," alisema.

Citibanamex, ni benki ya kampuni ya Citigroup Inc, na ilisema mfumo wake ulikuwa umewekwa kipimo cha umri na haungeweza kukubali umri wa Bi Félix.

Miguel Castro Reynoso, waziri wa ustawi katika jimbo la Jalisco, alimtembelea nyumbani kwake na kumpa pole.

Aliwashukuru wanahabari kwa kuangazia kisa hicho na kuahidi kwamba kisa kama hicho hakingetokea tena.

"Karibuni au baadaye, Mungu mwenyewe hutoa," alisema Bi Félix baada ya kupokea pesa hizo.

Reuters wanasema benki hiyo imeahidi kumpa kadi ya benki haraka iwezekanavyo.

Bi Felix atatimiza miaka 117 Julai kwa mujibu wa cheti chake cha kuzaliwa, ambacho maafisa wanasema ni cha kweli.

Anasema alibaki yatima akiwa na miaka saba.

Ameishi muda zaidi kuwashinda watoto wake sita kati ya 10 aliojaliwa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii