Waislamu watoa 'fatwa' dhidi ya ndoa za watoto Indonesia

Viongozi wa kike wa Kiislamu waliotoa agizo la fatwa dhidi ya ndoa za watoto Indonesia
Image caption Viongozi wa kike wa Kiislamu waliotoa agizo la fatwa dhidi ya ndoa za watoto Indonesia

Viongozi wa kike wa dini ya Kiislamu nchini Indonesia wametoa agizo la fatwa dhidi ya ndoa za mapema miongoni mwa watoto.

Agizo hilo ambalo halina uhalali wa kisheria lilitolewa baada ya mkutano wa siku tatu wa viongozi wa kike wa kidini katika taifa hilo.

Viongozi hao wametoa wito kwa serikali kupandisha umri wa wasichana wanaoolewa kutoka miaka 16 hadi 18.

Indonesia ni taifa lenye Waislamu wengi na lina idadi kuu ya watoto wanaoolewa duniani.

Kulingana na afisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulia maswala ya watoto UNICEF mmoja kati ya watoto 4 nchini Indoneasia huolewa kabla ya umri wa miaka 18.

Mkutano huo uliofanyika katika eneo la Cirebon kisiwani Java ndio mkutano mkuu wa kwanza kufanywa na viongozi wa kike wa dini ya Kiislamu.

Maagizo kama hayo hutolewa nchini Indonesia lakini hutolewa na baraza la Ulamaa, ikiwa ndio mamlaka kuu ya Kiislamu ambayo hushirikisha wanaume pekee.

''Viongozi wa dini wa kike wanajua maswala na changamoto ambazo huwakabili wanawake ,tunaweza kuchukua hatua bila kuisubiri serikali kuwalinda watoto hawa'', kulingana na mwandalizi wa mkutano huyo Ninik Rahayu.

Viongozi hao wa kidini wametaja tafiti ambazo zinaangazia kwamba watoto walioolewa hawaruhusiwi kuendelea na masomo yao hivyobasi nusu ya wanandoa hupeana talaka.